Akizungumza jana, Mtendaji wa Kata ya Lugubu, Dotto alisema hayo
yalitokea wakati yeye na mgambo watatu, Zengo Salum, Juma Gaston na
Luziga Kashindye walipokwenda kijijini hapo kufanya sensa ya mifugo kwa
baadhi ya wafugaji waliokuwa wamegoma kuhesabu mifugo yao.
Alisema wakiwa njiani wanakwenda, walipata taarifa kuwa kuna kaya
moja imeanika dawa za kulevya aina ya bangi kwenye kichanja cha miti
huku nyingine zikiwa zimelimwa katika mashamba ya familia hiyo.
Dotto alisema baada ya taarifa hiyo, walikwenda hadi kwenye mji huo
wa Sweya Nhunyula ambako walikuta bangi zaidi ya gunia moja ikiwa
imeanikwa.
Na walipokwenda shambani, walikuta michezo zaidi ya 103 iliyolimwa
katikati ya shamba huku ikiwa imezungukwa na mazao ya mahindi.
Alisema baada ya hapo, alipiga picha bangi hiyo huku wahusika wakiwa
wameshika mimea hiyo na baadaye walirudi nyumbani kwa watuhumiwa huku
akipiga simu Kituo cha Polisi Igunga.
Alifafanua kuwa, wakati yeye na wenzake wakiwasubiri polisi, ghafla
alijitokeza mama wa nyumba hiyo, Yunge Zengo na kutangaza kutokuwa
tayari kwenda polisi, ndipo Kaimu Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Gambo
Sweya ambaye ni mtoto wa Sweya Nhunyula alipoungana na nduguze
kuwashambulia kwa fimbo watendaji, kitendo kilichowafanya mgambo na
mtendaji wa kijiji kukimbia.
Anasema waliacha kumpiga baada ya kumwamuru akabidhi kitabu
alichokuwa ameandika majina yao pamoja na sahihi zao. Aliruhusiwa
kuondoka na pikipiki, bila kubeba dawa hizo.
Siku iliyofuata polisi walifika kijijini hapo na kukuta familia yote
ikiwa imehama huku bangi iliyong’olewa shambani ikiwa imefichwa.
Mtendaji huyo na Mtendaji wa Kijiji, James Martin wameripoti tukio
Polisi, ambayo kupitia kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Hamisi Selemani
imekiri kupata taarifa za tukio hilo.
chanzo:Habarileo.
Comments