
KAMATI ya Maendeleo ya Wanawake, Habari na Utalii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imevitaka vyombo vya Habari nchini kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa kufuata misingi ya weledi, maadili na miiko ya fani hiyo ili viweze kujenga uaminifu wa kudumu kwa jamii.
Wito huo umetolewa wakati Kamati hiyo ilipotembelea Bahari Fm Radio, na kukagua shughuli za kiutendaji na uendeshaji ndani ya taasisi hiyo, na kushauri taasisi hiyo kuandika na kutangaza habari za kudumisha Amani na Utulivu wa nchi sambamba na kupinga vitendo vya kuhamasisha vurugu.
Akizungumza baada ya kutembelea maeneo mbali mbali ya redio hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ali Suleiman Shihata ameupongeza uongozi wa Bahari fm na watendaji wake kutokana na kazi nzuri wanayoifanya ya kuelimisha na kuburudisha umma.
Alisema chombo hicho kimekuwa ni miongoni mwa taasisi bora za kihabari Visiwani Zanzibar, kutokana na umahiri wake wa kuandaa vipindi bora vinavyoendana na wakati wa sasa.
Pia alitoa wito kwa watendaji wa chombo hicho kutumia vizuri kalamu zao na kufanya kazi za kihabari kwa kuzingatia weledi, maadili, miiko na misingi ya fani hiyo ili taasisi hiyo iendelee kuwa na heshima na kuaminiwa na jamii.
Mapema Mkurugenzi wa Bahari FM Bw. Yusuph Omar Chunda kupitia ziara hiyo aliwashauri wajumbe wa kamati hiyo kudumisha ushirikiano uliopo baina ya serikali hasa baraza la wawakilishi na vyombo vya habari.
Ujumbe huo ulioongozana na Naibu waziri wa habari, utalii, utamaduni na michezo, Mh. Chuom Kombo Khamis, mbali na bahari FM pia wametembelea vituo kadhaa vya habari vya kibinafsi.
chanzo:zanzibar24.
Comments