Uvumilivu watakiwa kesi ya mke wa bilionea Msuya.

HAKIMU Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Thomas Simba amewataka washitakiwa wa kesi ya mauaji inayomkabili mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Mariam Mrita (41) na mfanyabiashara Revocatus Muyela (40), kuwa wavumilivu, kwa sababu anaandaa maamuzi yaliyotokana na mabishano ya kisheria.

Alitaka hivyo baada ya Wakili wa Serikali, Patrick Mwita kudai kuwa kesi hiyo imekuja kutajwa.

Alisema wanaahirisha kesi hiyo kwa muda mfupi ili kutoa uamuzi sahihi kutokana na mabishano ya kisheria kati ya upande wa mashitaka na mawakili wa utetezi kuhusu kufunguliwa upya kwa kesi hiyo.

Aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 11, mwaka huu kwa ajili ya kutoa uamuzi. Mawakili wa utetezi walidai kuwa kesi hiyo imefunguliwa kinyume cha sheria, hivyo ifutwe.

Awali, washitakiwa Mrita na Muyela waliachiwa huru na mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa kisha wakakamatwa tena na kusomewa upya mashitaka ya mauaji.

Katika kesi hiyo, washitakiwa hao wanatuhumiwa kumuua kwa makusudi Aneth Msuya ambaye ni dada wa bilionea Erasto Msuya. Mauaji hayo yanadaiwa kutendeka eneo la Kibada, Kigamboni jijini Dar es Salaam, Mei 25, mwaka jana.

Wakili wa washitakiwa, Peter Kibatala aliiomba mahakama kufuta kesi hiyo akidai kuwa imefunguliwa kinyume cha sheria, kwani ilishafutwa.

Alidai kuwa kesi hiyo imefunguliwa kinyume cha sheria kwa sababu ilishatolewa uamuzi Februari 23, mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa aliyewaachia huru washitakiwa wote.
Aidha, alidai kuwa mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kulipokea jalada hilo na kuwasomea washitakiwa mashitaka yao kwa kuwa limeshatolewa uamuzi.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Mutalemwa Kishenyi alipinga hoja hizo na kudai kuwa washitakiwa wamesomewa kosa hilo kwa mujibu wa sheria.

Alidai kuwa uamuzi uliotolewa ulikuwa ni kuwafutia mashitaka ambapo Jamhuri ina uwezo wa kuwakamata tena washitakiwa na kuwasomea kosa hilo la mauaji.

Pia haoni sehemu yoyote ambayo inaonesha kosa walilosomewa washitakiwa lipo kimakosa mahakamani hapo.
chanzo:Habarileo.

Comments