UN kuendelea kuiunga mkono Zanzibar kuimarisha miradi yake ya maendeleo.

UMOJA wa Mataifa (UN), umeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi yake ya maendeleo ikiwemo ile inayosimamiwa na Mashirika ya Umoja huo.

 Hayo yalielezwa na Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania ambaye pia, ni Mwakilishi Mkaazi wa Shrika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP Alvero Rodriguez akiwa amefuatana na viongozi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa wanaofanya kazi zao hapa Zanzibar ambao wapo hapa nchini kwa mkutano maalum wa kila mwaka unaofanywa na Umoja huo.


Mapema akitoa maelezo yake Mratibu huyo Mkaazi wa UN nchini Tanzania ambaye alifuatana na Wawakilishi Wakaazi wa Mashirika ya UN wanaofanya kazi zao hapa Tanzania alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa Serikali anayoiongoza kwa kusimamia vyema miradi ya maendeleo na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo.

Rodriguez alisema kuwa UN inathamini sana uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Tanzania ikiwemo Zanzibar, hivyo basi ni vyema hatua hizo zikaendelezwa kwa manufaa ya nchi na wananchi wake wote.

Katika maelezo yake Rodriguez alieleza kuwa UN imeamua kwa makusudi kuendelea kuunga mkono sekta za maendeleo zikiwemo elimu, afya, kilimo, mazingira, athari za tabia nchi, kupambana na umasikini pampja na unyanyasaji wa kijinsia kwa akina mama na watoto, changamoto ya ajira, na nyenginezo.

Aidha, alisema kuwa UN iko tayari kuendelea kuunga mkono seta hizo hasa ikizingatiwa kuwepo kwa madaliko makubwa ya kiuchumi duniani hatua ambayo inatoa nafasi kwa Umoja huo kuongeza nguvu kwa Mashirika yake kuendelea kusaidia nchi kama Tanzania ikiwemo Zanzibar.

Sambamba na hayo, kiongozi huyo wa UN nchini Tanzania alieleza hatua zinazoendelea katika kuiunga mkono Zanzibar katika hatua zake za Kukuza Uchumi na Kupambana na Umasikini na kutekeleza Dira 2020.

Nao ujumbe huo wa UN nchini Tanzania, kupitia Mashirika yake yalitoa pongezi kwa Dk. Shein kutokana na uongozi wake katika kuendeleza miradi ya maendeleo inayosimamiwa na mashirika hayo huku wakiahidi kuendelea kumuunga mkono.

Nae Rais Dk. Ali Mohamed Shein kwa upande wake alitoa pongezi kwa Umoja wa Mataifa kupitia mashirika yake kwa mashirikiano makubwa inayoyatoa kwa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza changamoto mbali mbali zilizopo katika sekta za maendeleo ikiwemo elimu, afya, ajira, unyanyasaji wa wanawake na watoto, athari za tabia na mambo mengineyo.

Hata hivyo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuueleza ujumbe huo wa UN kuwa mbali ya changamoto hizo Zanzibar haikufunga mikono na imekuwa ikichukua juhudi za makususdi katika kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi kwa mashirikiano ya Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa.

Dk. Shein alisema kuwa hatua mbali mbali zimekuwa zikichukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha sekta ya elimu kwa kuendelea na ujenzi wa skuli mpya za Msingi na Sekondari, Vyuo Vikuu. Aidha, alieleza namna Serikali ilivyoelekeza nguvu katika kilimo cha umwagiliaji maji.

Pia, alieleza juhudi zinazochukuliwa katika kuimarisha sekta ya afya,mafanikio yaliopatikana katika kupambana na Malaria, kupambana na unyanyasaji wa akina mama na watoto na kueleza mikakati mipya iliyowekwa na Serikali katika kupambana na kadhia hiyo hivi sasa.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa kuwepo kwa Ofisi za pamoja za Umoja wa Mataifa hapa Zanzibar ‘One UN’ kumeweza kurahisisha kwa kiasi kkkubwa ufanyaji kazi wa Mashirika hayo na kupelekea kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa zaidi.

Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na Mabalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliokuja kumuaga Rais, ambapo akitoa nasaha na maelekezo kwa Mabalozi hao, Dk. Shein alisema kuwa nchi zote wanazokwenda kufanya kazi Mabalozi hao ni muhimu na kuwataka kutambua kuwa katika ufanyaji kazi wao wajue kuwa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania ina pande mbili.

Alieleza haja ya kuimarisha uchumi wa kidiplomasia katika uwakilishi wao katika nchi watakazozifanyia kazi na kusisitiza kuwa katika suala zima la uchumi hivi sasa Tanzania imeweka kipaumbele sekta ya viwanda hivyo, ni vyema wakaitangaza ikiwa ni pamoja na kuwashajiisha wawekezaji kuja kuekeza hasa katika sekta ya viwanda.

Pamoja na hayo, alieleza haja kwa viongozi hao kuutangaza utalii wa Tanzania ambapo kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara sekta hiyo imeendelea kupewa kipaumbele kutokana na mchango wake mkubwa wa uchumi na pato la Taifa kwa ujumla.

Aidha, alisisitiza haja ya kuyashajiisha mashirika ya ndege kufanya safari zao hapa Tanzania yakiwemo mashirika ya ndege ya India, Ujerumani, Algeria na nchi nyenginezo huku akitilia mkazo umuhimu wa kuwasaisia wanafunzi ambao wanasoma katika nchi wanazoenda kuzifanyia kazi pale wanapokuwa na matatizo yao.

Nao Mabalozi hao walimshukuru Dk. Shein kwa nasaha na maelekezo yake na kuahidi kuyazingatia na kufanya kazi hasa suala zima la uzalendo katika Muungano.

Miongoni mwa Mabalozi hao ni Balozi Omar Yussuf Mzee anekwenda nchini Algeria, Balozi Abdalla Saleh Posi anenkwenda nchini Ujerumani, Balozi Baraka Luvanda anaekwenda India, Balozi Sylivester Ambukile anaekwenda nchini Afrika Kusini, Balozi Daudi Massima anekwenda nchini Israil na Balaozi Sylivester Massele Mabumba anaekwenda Umoja wa Visiwa vya Comoro.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
chanzo: zanzibar24.

Comments