Turathi 10 za Mwanamapinduzi Abeid Amaan Karume.

Wazanzibari, Watanzania na Dunia kwa ujumla tunaingia kwenye kumbukumbu muhimu za miaka 45 za Kiongozi Mweledi, Jasiri na Mwanamapinduzi Abeid Amaan Karume.
Mengi unayajua kuhusu mwanamapinduzi huyu, kindakindaki wa Bi Amina Bint Kadudu na mume wa wanawake kadhaa, Pili Bint Ahmed Ambari, Ashura Bint Maisara na Fatma Gulamhussein Ismail maarufu Fatma Karume.

Makala haya yanaangazia mambo 10 ambayo Mwanamapinduzi Abeid Amani Karume ameyaacha ikiwa ni urithi kwa vizazi vya Wazanzibari, Watanzania na Dunia kwa ujumla wake.
  • Mapinduzi ya Zanzibar 
Yataje popote, yaeleze utakavyoyaeleza, huwezi kuzungumza mafanikio ya mapambano ya usiku wa tarehe 11 Januari 1964 pale Bomani na maeneo mengine pamoja na mipango ya fete iliyohanikiza usiku huo Mjini na Mashamba, halafu ukasahau jina la Mwanamapinduzi Abeid Amani Karume.
Itakuwa ni ujuha kumuweka kando Karume , Mwanamapinduzi ambaye ndiye aliyekuja kuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri mpya ya Watu wa Zanzibar iliyozaliwa katika mapambazuko ya Tarehe 12 Januari 2014.
Urithi huu aliouacha Hayati, Mwanamapinduzi Karume ndiyo ulioleta uhuru wa kweli kwa Wazanzibari wote ukiupiga kumbo uhuru bandia kwa ajili ya tabaka la watu wachache aliokabidhiwa  Sultan aliyepinduliwa Jamshid bin Haroub bin Khalifa na Waziri mkuu wake Muhammad Shamte Hamad.
  • Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Baada ya Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964 Karume alitambua udugu uliopo baina ya wananchi wa Zanzibar na wenzao wa Tanganyika, hivyo hakuchelewa wala kuogopa kuwaunganisha watu wake na watu wa Tanganyika katika kuimarisha uhusiano wa wananchi wa pande mbili hizo.
Aliweka kando ubinafsi , ulafi wa madaraka na maslahi binafsi na kwa azma ya kuipenda nchi yake alikutana na Mwalimu Nyerere na kukubaliana kuhusu kuunganisha nchi zao . Hatimaye Tarehe 26 aprili 1964 Zanzibar ikaungana na Tanganyika kutengeneza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Urithi huu ni muhimu kwa kuendeleza uhusiano baina ya Wazanzibari na wenzao wa Tanganyika , faida nyingi zimepatikana katika urithi huu.

  • Majumba ya Maendeleo.
Kisiwani Unguja kuna eneo maarufu linaitwa Michenzani, Wazee wa zamani wanajua eneo hilo lilivyokuwa hapo awali likiwa na majina mengi tofauti tofauti, nyumba zilizokuwepo pia wanazikumbuka na mandhari ya eneo hilo kwa ujumla pia wanayakumbuka.
Nikukumbushe kitu muhimu kwenye kumbukumbu zako kwamba Tarehe 4 Mei 1970 Mwanamapinduzi Karume alizindua mradi mkubwa na muhimu wa majumba maarufu yaitwayo majumba ya Michenzani hivi sasa. Urefu wa Majumba hayo (siyo kwenda juu) yanasimuliwa kwa hadithi maarufu kwenye maskani na barza mbalimbali kwamba Mwanamapinduzi Karume alisimama pale lilipoanza jumba namba moja na kukamata kamba halafu akamwambia Mwanamapinduzi mwenzake Thabit Kombo Jecha achukue kamba akimbie nayo mpaka akawa hamuoni akamwita wee Thabit panatosha hapo.
Hapo ndio ulikuwa mwanzo wa urithi muhimu uliotapaa maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba wa ujenzi wa Majumba ya Maendeleo aliotuachia Karume. Jumba lile la mwanzo liligharimu jumla ya shilingi Milioni nne laki saba na hamsini na mbili elfu na lina fleti 132.
  • Elimu bila Malipo
Wanataaluma wengi wanakubaliana na msemo maarufu kwamba ukitaka kumtawala mtu mnyime elimu, hivyo ndivyo ilivyofanyika kwa muda mrefu katika visiwa vya Zanzibar , tawala zilizopita kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964 zilifunga mlango wa elimu kwa wananchi walio wengi hali iliyopelekea Wazanzibari wengi kukosa elimu.
Miezi tisa baada ya Mapinduzi, Mzee Karume fawahisha alitangaza elimu bila malipo kwa Wazanzibari wote, Moja ya hotuba zake akisisitiza suala la umuhimu wa elimu akiwaasa walimu kuwasomesha wanafunzi kwa umakini na kuhakikisha kila mwanafunzi anafahamu alichosomeshwa.
Hii leo kila ifikapo Septemba 23 ya kila mwaka Wazanzibari, wanataaluma hukumbuka tamko hilo lililowagomboa watu wengi kielimu na baadhi yao kuwa na kibri walichonacho hivi sasa.
  • Matibabu bure 
Moja ya matangazo yaliyotoka mapema kabisa baada ya Mapinduzi ni Tangazo la Matibabu bure lililotangazwa Tarehe 23 Machi 1964 . Hii ilimaanisha kwamba Wazanzibari wa hali zote wasiwe na wasiwasi kuhusu afya zao.
Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja na hospitali nyenginezo zilipewa kila kitu katika kuhakikisha zinatoa matibabu bora kwa wananchi wa visiwa vyetu.
Urithi huu ndio chachu ya kuenea huduma za afya hivi sasa katika maeneo yote ya mijini na mashamba Unguja na Pemba.
  • Ugawaji wa Ardhi Eka Tatu
Tarehe 8 Machi 1964 Karume alitangaza kwa Wazanzibari kwamba Watagaiwa ardhi eka tatu tatu Unguja na Pemba. Siku nne baadae Machi 11 1964 Zoezi la ugawaji wa Ardhi wa eka tatu kwa kila Mwananchi lilianza katika eneo la Dole Unguja.
Nikujuvye kitu kwamba kabla ya Mapinduzi sehemu kubwa ya ardhi ya Zanzibar ilikuwa inamilikiwa na mabwanyenye wa kihindi na wakiarabu pamoja na tabaka la tawala.
Kama si Mapinduzi na fikra za Karume Zanzibar ingekuwa kama Zimbabwe katika suala la Ardhi , mabwanyenye wachache wangekuwa wanamiliki ardhi na wananchi wangekuwa wanaishi katika ardhi za mabwanyenye hao.
  • Mwanzilishi wa vyama vya Wafanyakazi
Mzee Karume alikuwa Muafrika wa kwanza kuanzisha chama cha wafanyakazi kilichotambulika kama jumuiya ya mabaharia wa Unguja na Pemba ambacho kilisajiliwa mwaka 1949. Mwanzilishi mwengine wa chama hicho alikwa Bakari Jabu.
  • Ndoa za kuondoa ukabila na ubaguzi
Tofauti na tafsiri ya watu wengi Mzee Karume alikuwa na nia njema kwenye ndoa hizi akiwa na lengo la kuondoa ubaguzi na ukabila uliokuwa umetamalaki kwa zaidi ya miaka 100 Visiwani humu kukiwa hakuna utengamano wa kijamii baadhi ya jamii zilijiona bora dhidi ya jamii nyengine.
Leo hii kutokana na ndoa hizo hakuna jamii ya kizanzibari isiyokuwa na uhusiano na jamii nyenginezo kidamu ambapo awali jamii hizo hazikuwa na uhusiano wa kidamu zaidi wa kibwana na kitwana.
  • Uwanja wa Michezo wa Amani (Amaan Stadium)
Mwaka 1970 Uwanja wa michezo wenye taa za kisasa za kuchezea mpira wa miguu wakati wa usiku ulifunguliwa Zanzibar ukiwa ni miongoni mwa viwanja bora Afrika. Kumbukumbu zinaeleza ulikuwa ni uwanja wa pili au watatu kwa ubora Afrika ukipitwa na viwanja vya michezo kilichpo Misri na Afrika Kusini.
  • Yanga na Simba
Simba leo hii isingeitwa Simba ingebaki na jina lake la Sunderland tu kama si Hayati Karume. Pengine makao makuu ya Yanga pale mitaa ya Jangwani na Twiga yasingekuwa kwenye jengo lile liliopo sasa lililonakshiwa kwa rangi za Njano na Kijani kama si Hayati Karume.
Sina haja ya kudadavua mengi kwa kiswahili cha leo itoshe tu kujua Yanga na Simba ni Turathi ya Hayati Karume.
 chanzo:zanzibar24.

Comments