Dk Tulia alitoa msimamo huo wakati akijibu mwongozo wa wabunge watatu
waliosimama mara baada ya kipindi cha maswali na majibu wakihoji
msimamo wa kiti cha Spika katika mwendelezo wa vitendo vya kutekwa kwa
watu mbalimbali, mmoja akidai wabunge 11 wamo katika mpango wa kutekwa.
Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe (CCM) na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph
Mbilinyi (Chadema) walitumia Kanuni ya 47 kuomba mwongozo kwa suala
hilo huku Mbunge wa Viti Maalumu, Devotha Minja (Chadema) akitumia
Kanuni ya 68 (7).
Katika ombi lake la mwongozo, Bashe aliomba Bunge kuahirisha shughuli
zake za jana ili kujadili vitendo vya utekaji wa watu huku akisema
anazo taarifa kutoka kwa mawaziri (bila kuwataja) kuwa kuna orodha ya
wabunge 11 walio katika mpango wa kutekwa.
“Mheshimiwa Naibu Spika natumia Kanuni ya 47 kanuni ndogo ya (1), (2)
na (3) na wewe unaweza kutumia kanuni ndogo ya (4) ili kuruhusu
shughuli za Bunge ziahirishwe ili kujadili suala la kutekwa ovyo kwa
watu.
“Kipo kikundi cha watu ambacho hakijafahamika, kimekuwa kikiteka
watu. Kikundi hiki kilimteka Msukuma (Joseph Kasheku Msukuma – Mbunge wa
Geita Vijijini), kilimteka Bashe na pia Malima (Adam) wakati wa
mikutano ya CCM.
“Kikundi hiki nadhani ndicho pia kilichomteka Ben Saanane (Msaidizi
wa Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe), na juzi kilimteka msanii Roma
Mkatoli (Ibrahim Mussa – msanii maarufu wa Hip Hop).
Naomba suala hili lichukuliwe kama jambo la dharura na Bunge
liahirishe shughuli zake ili tujadili suala hili ambalo limeanza kuwatia
hofu Watanzania,” alisema Bashe na kuongeza: “Nasema hivyo kwa sababu
hatujui ni Watanzania wangapi wa ngazi za chini wametekwa na kikundi
hiki hadi sasa.
Wapo baadhi ya mawaziri wameniambia kuna orodha ya wabunge kumi na
moja walio katika orodha ya kutekwa nikiwemo mimi na wameniambia niwe
makini niwapo barabarani.
“Chama changu cha CCM kiliomba ridhaa kwa Watanzania ili kuwaongoza
na si kuwahatarishia maisha. Naomba Bunge liunde Tume au tutumie Kamati
yetu ya Bunge ya Usalama ili kuchunguza suala hili. Hali si salama,
hakuna hope (matumaini).”
Naye Mbilinyi akiomba mwongozo kwa suala hilo alisema; “Taifa lipo
gizani, kumezuka utamaduni mpya, utamaduni wa kimafia, ni utaratibu
uliokuwepo miaka ya zamani sana wakati ule alitekwa Kassim Hanga
Zanzibar, lakini ukatoweka, na sasa umerudi.
“Tangu utamaduni huu uanze Jeshi la Polisi wamekuwa wanasema hawajui
waliko watu waliotekwa. Lipo tukio la kutowekwa Ben Saanane, tukio la
kukutwa kwa maiti za watu sita au saba kwenye viroba katika Mto Ruvu na
wakazikwa bila kufanyiwa uchunguzi.
“Nape (Nnauye – Mbunge wa Mtama) naye alitekwa na mtu mwenye bastola
bahati nzuri akaokolewa na Maulid Kitenge (mtangazaji wa E FM).
“Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani (Mwigulu Nchemba) kama mambo
yanafanyika na hupewi taarifa au unashinikizwa, ni vizuri ukajiuzulu.
Wewe ni mtu wa kiwango cha juu maana uligombea urais na bado una
future mbele yako, unaweza kujiuzulu na siku za usoni ukawa Rais.
“Rais Mwinyi (Ali Hassan – Rais mstaafu) aliwahi kujiuzulu miaka ya
1976 kwa makosa yaliyofanywa na watendaji wa chini yake lakini akarudi
kama shujaa miaka ya 1980 na kuwa Rais wa nchi hii. Na wewe kwanini
usifanye hivyo ili kulinda heshima yako?” alihoji Mbilinyi.
Naye Minja akitumia Kanuni namba 68 (7) aliomba mwongozo wa Naibu
Spika akisema saa 5 asubuhi juzi, askari wenye silaha za moto walivamia
na kuzingira nyumba yake iliyopo mjini Morogoro wakiwa na lengo la
kumkamata mbunge huyo.
Alisema polisi hao walifanya hivyo pasipo kumpa taarifa yeye ambaye
ni kiongozi na kuwa hatua hiyo imeleta tafrani na sintofahamu kwa
familia yake pamoja na kuwa hawakumkamata kutokana na kuwa bungeni mjini
hapa.
Akijibu mwongozi wa Bashe na Mbilinyi, Naibu Spika Dk Tulia alisema
isingewezekana kwa Bunge kuahirisha shughuli zake ili kujadili suala
hilo kwa vile vyombo vya sheria vinashughulikia suala hilo.
Alisema kimsingi ili kuielewa kanuni ya 47 iliyotumiwa na wabunge
katika kuomba mwongozo huo, ni lazima kanuni hiyo isomwe na kanuni ya 48
kifungu kidogo cha 4 kinachofafanua ni jambo lipi linaweza kuhesabiwa
na Bunge kuwa ni la dharura.
Alisema kanuni hiyo inafafanua vizuri kwamba jambo litahesabika kuwa
ni la dharura endapo litakuwa na maslahi kwa taifa na litakuwa
halijashughulikiwa na vyombo vya kisheria na kwamba jambo la utekaji
nyara kwa wananchi si la dharura kwa vile linashughulikiwa na vyombo ya
sheria na utaratibu wa kawaida wa kisheria utatumika katika
kulishughulikia.
Kuhusu mwongozo wa kuvamiwa kwa makazi ya Mbunge Minja, Naibu Spika
alisema asingeweza kulitolea mwongozo kwa vile kwa mujibu wa Kanuni ya
67 (8) Spika anapaswa kutolea mwongozo kwa suala ambalo limetokea mapema
bungeni.
Comments