Sumatra: Vyombo vya kuvulia samaki ni duni.

 Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), imesema uduni wa vyombo vya kuvulia pamoja na ujuzi mdogo ndio tatizo linalosababisha Tanzania kutofanya uvuvi wa kibiashara katika kukuza uchumi.

Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe alisema hayo wakati akizindua mafunzo ya usalama kwa waendeshaji wa boti ndogo katika Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) uliopo Mbegani wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.


Ngewe alisema kuanza kwa mafunzo ya usalama kwa waendesha boti ni jambo muhimu litakalowezesha kuimarisha sekta ya uvuvi, lakini pia kutoa ujuzi kwa mabaharia waliopo nchini.

Alisema ili kutekelezwa kwa sera ya Tanzania ya viwanda yapasa kuwepo kwa mafunzo hayo ya usalama katika ukanda wa bahari na hata katika maziwa, jambo litakalosaidia kuongezeka kwa ajira kwa vijana walio wengi, lakini pia kuimarika kwa lishe na afya ya Watanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra alieleza kuwa kwa kuimarishwa kwa sekta ya uvuvi, itasaidia Tanzania kusafirisha mazao ya samaki kutoka Bahari Kuu hadi katika viwanda vyenye kuchakata samaki kama ambavyo nchi za nje hufanya na kusaidia kuimarisha uchumi wa eneo lao.

Alisema mafunzo hayo pia yatasaidia vijana wa Kitanzania ambao ni mabaharia kuingia katika meli kubwa, na kutokana na ujuzi watakaoupata wataleta maendeleo nchini.

Awali, Mtendaji Mkuu wa FETA, Yahya Mgawe alisema sababu ya mafunzo hayo inatokana na kuwepo kwa ajali nyingi za majini na wakati mwingine kuhatarisha maisha ya walio wengi.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabaharia nchini, Frank Chuma alisema mafunzo hayo yatasaidia kuinua hadhi ya mabaharia nchini kwa kuwa walisahaulika na kuonekana wasioweza kupata ajira kutokana na wengi wao kutokupita katika vyuo vinavyotambulika.
chanzo:Habarileo.

Comments