SPIKA wa Bunge, Job Ndugai ameamuru kufikishwa katika Kamati ya Kudumu ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kwa Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee kwa kuonesha vitendo vya utovu wa nidhamu.
Spika Ndugai pia alilifahamisha Bunge kuwa kamati hiyo jana ilifanya kazi ya kumhoji Mkuu wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Alexander Mnyeti baada ya kukamilisha kazi ya kumhoji Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Katika amri yake, Spika Ndugai amemtaka Mdee ambaye yupo nje ya mji wa Dodoma kuwa amewasili mjini hapa hadi kufikia saa 4.23 asubuhi leo ili kukutana na kamati hiyo vinginevyo Jeshi la Polisi limkamate popote pale alipo na afikishwe Dodoma akiwa amefungwa pingu.
Kuhusu Mbowe, Spika alimuagiza awe amefika katika kamati hiyo ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge jana na kuwa kinyume chake hatua zingine zitachukuliwa dhidi yake.
Spika alitangaza hayo bungeni jana wakati akitoa majibu ya miongozo iliyoombwa na Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) na Mbunge wa Madaba, Joseph Mhagama (CCM) ambao wote waliomba mwongozo kujua Spika anasemaje kuhusu vitendo vya utovu wa nidhamu uliofanywa na wabunge hao.
Wanadaiwa kufanya vitendo hivyo wakati na baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa wagombea wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) uliofanyika Aprili 4, mwaka huu.
Lugola katika maelezo yake ya mwongozo, alisema kuna rekodi ya video (clip) inazunguka katika mitandao ya jamii, ikimuonesha Mbowe akitukana Spika, Bunge na Chama Cha Mapinduzi huku kiongozi wa taifa wa chama hicho akiwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli.
“Mheshimiwa Spika Mbowe analitukana Bunge na Rais wakati uchaguzi huu wote tumeshuhudia kuwa ulikuwa ni wa kidemokrasia. Wote tulishuhudia kuwa tuligawiwa vitabu vya kupiga kura vyenye orodha ya wagombea wote ambapo wagombea wawili wa Chadema walishindwa.“Sasa hatua hii ya kiongozi wa chama kutuita wabunge kuwa ni wajinga, wapuuzi na hatuna maana inatoka wapi? Hivi ni ruksa kwa kiongozi wa chama cha siasa kulinajisi au kulitukana Bunge hili kwa kufanya shughuli zake za kibunge?” Alihoji.
Naye Mhagama katika mwongozo wake kwa Spika akitumia kanuni ya 68 (7) sawa na wenzake aliomba kujua msimamo wa Spika kwa Mbunge (Mbowe) anapotoa matusi dhidi ya Spika na Bunge na kumdhalilisha Rais na Waziri Mkuu.
Akijibu, Spika Ndugai alisema pamoja na kanda hiyo inayomuonesha Mbowe ipo pia inayomuonesha Mdee akionesha vitendo vya utovu wa nidhamu dhidi ya Spika.
“Watanzania wengi wamesikitishwa sana na jambo hili, si utamaduni wetu Watanzania kutoa lugha za matusi. Na hii si mara ya kwanza kwa Halima kuonesha utovu kama huu wa nidhamu. Siku ile nilivumilia sana...nikaomba Mungu anisaidie. Sasa naagiza suala lake liwasilishwe kwenye Kamati yetu ya Maadili.
“Haiwezekani Bunge likawa linaita watu wa nje ili kuwahoji kwa utovu wa nidhamu halafu tukaacha wabunge wanafanya vitendo hivi. Naagiza afike mara moja najua hayupo Dodoma, lakini hadi kesho kwenye muda kama huu (saa 4.23) awe amewasili au vinginevyo naagiza Jeshi la Polisi kumkamata popote pale alipo na aletwe Dodoma na pingu,” alisema Spika Ndugai.
Akimzungumzia Mbowe, Spika Ndugai alisema; “Kumhusu Freeman Mbowe suala lake naliwasilisha kwenye Kamati ya Maadili ili wakalishughulikie kwa taratibu zao. Naagiza awe amefika kwenye kamati hii leo, vinginevyo hatua zitachukuliwa.
“Wabunge kama mnavyojua kamati hii imemaliza kazi ya kumhoji Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (Makonda) na leo hii itamhoji Mkuu wa Wilaya ya Arumeru (Mnyeti). Naagiza wajumbe wa kamati wakafanye kazi hiyo sasa,” alieleza Spika Ndugai.
Katika hatua nyingine, Umoja wa Wanawake wa CCM umelaani kitendo cha Mbowe na Mdee ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chadema (Bawacha) kutoa lugha za utovu wa nidhamu kwa Spika Ndugai na kusema kitendo hicho hakikubaliki.
Katibu Mkuu wa UWT Taifa, Amina Makilagi aliyasema hayo katika moja ya kumbi za mikutano za Bunge mjini hapa jana. “Tunalaani kauli za matusi na kejeli za Mbowe kwa Rais Magufuli, kwa Waziri Mkuu, Spika na sisi wabunge.
Hatukutegemea kwa kiongozi anayeheshimika na Watanzania kama Mbowe kutoa lugha kama hizi za matusi na kejeli dhidi ya viongozi wetu.Tunamtaka Mbowe aombe radhi kwa Rais, Bunge na Watanzania.
“Tunalaani pia kitendo cha Mdee ambaye ni Mwenyekiti wa Bawacha kutoa lugha za matusi. Wanawake tunatarajiwa siku zote kuwa ni mfano katika jamii. Mwanamke wa Tanzania anatakiwa kuwa mtu mwenye staha na si kutoa matusi kama hivi,” alieleza.
Akizungumzia kuitwa kwenye Kamati hiyo ya Bunge, Mbowe alisema kuitwa kwenye kamati hiyo ni jambo la kawaida hivyo atafika ili kusikiliza anachoitiwa.
“Siwezi kusema mambo mengi kwa sababu wakati Spika (Ndugai) anatoa agizo lake mimi sikuwepo bungeni na hivyo sijui ni mashitaka gani wanayonishitaki huko. Nitakwenda ili kusikia wananiitia nini maana kuitwa kwenye Kamati hiyo ni jambo la kawaida kwa mbunge,” alisema Mbowe kwa kifupi.
chanzo:Habarileo.
Comments