SERA ya Elimu Bure iliyoanza kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano kuanzia mapema mwaka huu imeelezwa kuwa imewapunguzia mzigo mkubwa wazazi na walezi hususani katika jamii masikini kuweza kusomesha watoto wao.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari(Maelezo), Dk Hassan Abbas alitoa ufafanuzi kwamba juhudi za makusudi zilizofanywa na serikali ya kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari zimeanza kutoa matunda yaliyotarajiwa kiasi kwamba shule hizo sasa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi kuliko kabla ya hatua hiyo.
Dk Abbas alikuwa anatoa ufafanuzi kuhusu taarifa zilizoandikwa na baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni vikibeza mafanikio yanayoonekana kuendelea kupatikana baada ya kuanza kwa sera ya elimu bure ambapo serikali kila mwezi hutenga Sh bilioni 18 kwa ajili hiyo.
‘’Sera ya elimu bure imekuwa mkombozi na faraja kubwa kwa watanzania na changamoto zilizojitokeza zinaendelea kushughulikiwa na serikali kwa umakini unaostahili,’’ alifafanua Dk Abbas.
Kuanzia Januari mwaka huu, elimu ya shule ya msingi na sekondari katika shule za serikali inatolewa bure bila kulipa ada na gharama za mitihani kama ilivyokuwa hapo awali.
Dk Abbas alisema kabla ya sera hiyo serikali ilikuwa inatoa ruzuki kwa shule hizo lakini ilikuwa inapatikana kati ya asilimia 60 hadi 70 tu.
‘’Ripoti tulizonazo sasa baada ya kuanza kwa Sera ya Elimu Bure upatikanaji wa fedha kwa ajili ya shule za msingi na sekondari umefikia asilimia 95 na tena zinatolewa kwa uwazi zaidi tofauti na hapo awali,’’ alifafanua.
Alisema kutokana na kuwatua mzigo wa ada za shule na michango mbalimbali wazazi na walezi wamehamasika kuwaandikisha kwa wingi watoto kujiunga na shule za msingi na wale waliofauli kujiunga na sekondari kwenda kusoma katika shule hizo pasipo vikwazo vya ada na michango.
chanzo:Habarileo.
Comments