Safari kuondoa malori Dar yaiva.

UJENZI wa Bandari Kavu ya Ruvu unaofanywa na Shirika la Uchumi la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) umekamilika katika awamu ya kwanza.

Hata hivyo, bandari hiyo ambayo inaelezwa kuwa itasaidia kupunguza msongamano wa malori katika Jiji la Dar es Salaam, inatarajia kuanza kutoa huduma Julai mwaka huu, baada ya kukamilika hatua ya pili ambayo ni ujenzi wa miundombinu mingine ndani ya bandari hiyo.


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Deusdedit Kakoko aliliambia gazeti hili kuwa kazi ambayo Suma JKT walikabidhiwa wameshaikamilisha na sasa hatua inayofuata ni ujenzi wa miundombinu mingine ndani ya bandari hiyo kavu.

“Nina imani kuwa shughuli zote zitakamilika hivi karibuni na bandari hiyo itaanza kutoa huduma zake mwezi Julai,” alisema Kakoko. Alisema ujenzi wa majengo ndani ya bandari hiyo kavu utafanywa na kampuni ambazo zitaiendesha ICD hiyo.

Alisema kwa sasa TPA inaangalia uwezekano wa kuingia ubia na wawekezaji wa sekta binafsi katika kujenga majengo ndani ya eneo hilo na kuiendesha.

Alisema pia kuwa ili kuleta ufanisi, TPA inafikiria kuwahusisha sekta binafsi ili wagawiwe maeneo ndani ya eneo hilo ili waiendeshe kwa pamoja.

Alisema hata hivyo suala hilo litatekelezwa iwapo atapata baraka za mamlaka za juu za serikali.

Mkurugenzi huyo alisema ujenzi mwingine utakaofanyika katika eneo hilo ni wa tuta la reli na ujenzi wa reli yenyewe ambao utatoka ilipo Reli ya Kati na kuunganisha na bandari hiyo kavu.

Alisema ujenzi wa tuta wataufanya Suma JKT wakati ujenzi wa reli utafanywa na kampuni inayojenga miundombinu ya Reli.

Alisema tayari TRL imeshatoa mchoro wa ujenzi wa reli hiyo na wanasubiri gharama za ujenzi wa reli hiyo pamoja na tuta.
“Kwa sasa ndio kwanza tunataka kwenda kufanya majadiliano, hatujajua gharama halisi za ujenzi wa reli hiyo,” alieleza mkurugenzi huyo.

Mwanasheria wa JKT, Kanali John Mbungo alisema kazi waliyokuwa wamekabidhiwa wameshaikamilisha na zimebaki shughuli ndogo ndogo wanazoendelea kuzikamilisha.

Alitaja kazi hizo kuwa ni kusafisha eneo hilo la ekari 500 kwa kufyeka msitu, kusakafikia ardhi na kushindilia kokoto.

Alisema kazi hiyo ilikuwa ni kubwa, lakini kwa kuwa wana utaalamu mkubwa walifanikisha ujenzi huo wa awali ndani ya muda waliopewa na serikali.

Alisema Suma JKT ingefurahi kama ingepewa zabuni nyingine ya kujenga majengo ndani ya ICD hiyo.

“Sisi kwa kweli kazi  yetu tumekamilisha, ila kuna kazi ya kujenga majengo ndani ya eneo hilo, tungefurahi kama wangetupatia kazi hiyo, lakini kwa sasa hatujui nani atapewa,” alieleza Kanali Mbungo.

Akizungumza wakati wa kutia saini makubaliano ya ujenzi wa ICD hiyo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema ujenzi wake unalenga kupunguza msongamano wa malori jijini Dar es Salaam na
ungekamilika ndani ya wiki tisa.

Profesa Mbarawa alisema ujenzi wa ICD hiyo utagharimu Sh bilioni 7.3 na utakapokamilika, makontena yote yatapelekwa kwenye bandari hiyo ya Ruvu kwa reli na malorii yanayotoka mikoani na nchi jirani yatakuwa yanachukulia mzigo wake katika huko badala ya kuja Dar es Salaam.
chanzo:Habarileo.

Comments