
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mkutano na Waalimu
wa Skuli za Sekondari kwa skuli za Mikoa yote miwili ya Pemba, huko
katika ukumbi wa Fidel Castro, Mkoa wa Kusini Pemba.
Katika maelezo yake Dk. Shein alieleza kuwa changamoto nyingi ambazo
zimekuwa zikiikabili sekta ya elimu tayari zimeshaanza kufanyiwa kazi na
Serikali anayoiongoza hatua ambayo ni uthibitisho kwamba Serikali ina
dhamira ya dhati katika kuimarisha sekta ya elimu pamoja na sekta
nyengine za maendeleo hapa nchini.
Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutatua
changamoto hizo kwa mujibu wa fedha zilizopo Serikalini ili kufanikisha
utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu 2016/2020, Ilani ya Uchaguzi
ya CCM 2015-2020, Mpango wa MKUZA III pamoja na mipango mengine ya
maendeleo ya Kitaifa na Kimataifa.
Dk. Shein alisisitiza kuwa Serikali itaweka kipaumbele maalum katika
kuimarisha mazingira ya kufanya kazi walimu ili yawe bora zaidi ambapo
itahakikisha muundo wa utumishi wa Wizara ya Elimu unafanyiwa kazi ili
kila mfanyakazi wakiwemo walimu wapate stahiki zao kwa mujibu wa sifa za
kitaaluma, uzoefu na dhamana zao.
Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa waalimu wote
wa Sekondari hapa Zanzibar kwa kupelekea kuongezeka kiwango cha ufaulu
wa wanafunzi wa Kidato cha Pili, Kidato cha Nne na cha Sita .
Dk. Shein pia, alitoa pongezi kwa dhati waalimu hao kwa matokeo ya
mtihani ya mwaka 2015, 2016 licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto
lakini matokeo yalikuwa mazuri na ya kupigiwa mfano.
Aliongeza kuwa hatua hiyo inatokana na kuwepo kwa elimu bure jambo
ambalo limeasisiwa na Rais wa Mwanzo wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume mara tu baada ya Mapinduzi
ambapo pia, katika Ilani ya chama cha ASP elimu bure ilitiliwa mkazo.
Aidha, Dk. Shein aliwataka waalimu hao kufuata maadili ya kazi yao
kwani kazi yao ni kazi iliyotukuka na wanaheshima kubwa katika jamii na
kuwapongeza kwa kuchagua kazi hiyio ya uwalimu ambayo ni kazi yenye
thawabu nyingi sana.
Pia, Dk. Shein alisisitiza haja kwa walimu kuwa na mbinu bora za
kufundishia na kuwasaidia wanafunzi ikiwa ni pamoja na walimu kujiandaa
kabla ya kufundisha na vile vile wawe tayari kujiendeleza kitaaluma na
kujifunza kwa wengine wanaofanya vizuri.
Dk. Shein alisema kuwa kwa bahati mbaya katika baadhi ya skuli wapo
walimu wachache wanaofanya kazi kwa kutegea kuwepo baadhi ya walimu
wanaoingiza siasa katika kufundisha kwao jambo ambalo ni kinyume na
wajibu na maadili ya uwalimu.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja kwa waalimu wakuu
kusimamia mazingira bora katika skuli kwa lengo la kupata matokeo mazuri
sambamba na kusisitiza haja kwa walimu kuimarisha michezo katika skuli
zao kwani Serikali imeanzisha Idara ya Michezo na Utamaduni kwenye
Wizara ya Elimu kwa malengo maalum.
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwataka waalimu hao kupeleka salamu kwa
jamii kuwa Srerikali imeamua kupambana na udhalilishaji wa wanawake na
watoto na wale wote watakaokamatwa kwa kujihusisha na kosa hilo hakuna
dhamana hadi kutakapotolewa hukumu.
Nae Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mmanga Mjengo Mjawiri
alisisitiza haja kwa waalimu kuwa wabunifu, kuwana na amadili pamoja na
heshima na kufuata muelekeo na mwennendo wan chi.
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Khadija Bakari Juma kwa niaba ya
walimu na Wizara alitumia fursa hiyo kuungana na wananchi kumpongeza Dk.
Shein kwa kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wake katika kipindi cha Pili
na kueleza mafanikio yaliopatikana katika sekta hiyo ya elimu ikiwa ni
pamoja na ongezeko la skuli, madarasa, vitabu, vifaa vyenginevyo.
Katibu Mkuu huyo pia, alieleza kuwa Wizara hiyo ina kauli mbiu ya
“Elimu Bora Kwanza” ikiwa ni msisitizo wa ubora wa elimu kwa wananfunzi
wote na kueleza kuwa tayari Serikali imeshakamilisha ujenzi wa Skuli ya
Msingi ya Mgonjoni, Skuli ya Sekondari ya Mohammed Juma Pindua ya
Mkanyageni na Skuli ya Kwarara ambayo ina kituo cha kurushia matangazo
ya redio na televisheni.
Aidha, alisema kuwa Serikali imeshatangaza zabuni za ujenzi wa skuli
tisa za ghorofa zikiwemo skuli tano kwa upande wa Unguja na nne kwa
upande wa Pemba huku akieleza kuwa mchakato wa kumpata mkandarasi
mwengine wa kuendeleza ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Kibuteni
umekamilika na mkataba wa ujenzi unatarajiwa kusainiwa hivi karibuni.
Bi Khadija alieleza mafanikio zaidi yaliopatikana katika kiwango cha
ufaulu katika mitihani ya taifa katika ngazi ya Kidato cha Pili, Kidato
ca Nnne na Kidato cha Sita pamoja na ongezeko la wanafunzi waliopatiwa
mikopo kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar pamoja na mambo
mengineyo katika sekta hiyo ya elimu.
Nao walimu hao walipata nafasi Ya kutoa risala zao kwa kila mkoa
ndani ya mikoa yote miwili ya Pemba na kueleza mafanikio yaliopatikana
katika sekta hiyo ya elimu pamoja na kueleza changamoto zilizopo.
Walimu hao pia, walipata fursa ya kutoa michago yao, maoni na ushauri
kwa Dk. Shein kwa lengo la kuimarisha sekta elimu hapa nchini huku
wakitoa pongezi zao kwa Rais Dk. Shein kwa kupata mshahara kwa wakati
muwafaka.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk.
chanzo:zanzibar24.
Comments