RAIS Dk. John Magufuli anatarajiwa kufungua kongamano la maadili lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).
Akizungumza
kwa niaba ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu Aboubakar Zuberi Mwenyekiti
wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Khamis Mataka, alisema kongamano
hilo litafanyika Aprili 24.
“Kongamano
hili limeandaliwa na Bakwata ambapo litahudhuriwa na masheikh
mbalimbali pamoja na viongozi wa kidini kutoka mikoa mbalimbali, lengo
likiwa ni kuangalia jinsi maadili yalivyoporomoka na kutafuta mbinu ya
kuijenga jamii iliyo bora,” alisema Sheikh Mataka.
Alisema kongamano hilo la siku moja litafungwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Alisema
wengine watakaohudhuria kongamano hilo ni wajumbe wa Ulamaa Taifa,
masheikh kutoka taasisi mbalimbali, viongozi wa kidini kanda, mabalozi,
wakuu wa vyombo vya usalama na wananchi walioalikwa.
Sheikh Mataka alisisitiza kuwa maadili ni muhimu ndani ya jamii na kwamba kwa sasa nchi inakabiliwa na mmomonyoko wa maadili.
“Ukiona
jamii inazungukwa na walevi, watumiaji dawa za kulevya, binadamu
wengine wanafurahia wenzao wakiuawa au kupata ajali, ni hali ya kupoteza
mwelekeo wa maadili,” alisema Sheikh Mataka.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments