Polisi Tanzania yaanzisha operesheni maalum baada ya kuuawa polisi 8.


Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amelaani mauaji ya askari polisi wanane wa nchi hiyo waliouawa kwa kushambuliwa na watu wenye silaha siku ya Alhamisi katika eneo la Jaribu Mpakani, Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani nchini humo, huku polisi ikianzisha operesheni maalumu kufuatia mauaji hayo.


Magufuli amesema ameshtushwa na kusikitishwa sana na vifo vya askari hao waliokuwa wanalitumikia taifa. Wakati huohuo, watu wanne wanaosadikiwa kuhusika na mauaji hayo ya askari polisi wanane na uporaji wa silaha wameuawa na polisi wakati wa operesheni iliyofanywa baada ya tukio hilo.

Aidha, Jeshi la Polisi limetaja chanzo cha mauaji ya askari polisi kujirudia mara kwa mara katika maeneo hayo ya kuanzia Mkuranga, Rufiji, Ikwiriri na Kibiti licha ya kuwa ni maeneo yenye watu wachache, kuwa ni mapori makubwa ambayo hutoa mwanya kwa watu wenye nia mbaya kujificha.
Akizungumza kuhusu tukio hilo katika Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya alisema baada ya majambazi kuwaua askari hao walipora bunduki saba na kutokomea kusikojulikana.

chanzo:parstoday.

Comments