Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yakabidhi Vitabu vya Sheria mbalimbali kwa Idara ya Mahakama Zanzibar.

Vitabu hivyo vya Sheria vitaanza kutumika rasmi katika mahakama ikiwa
ni mwendelezo wa kuzifanyia marekebisho sheria ambazo zimepitwa na
wakati.
Mkuu wa kitengo cha uandishi wa Sheria Saleh Said Mubarak kwa niaba
ya Mwanasheria mkuu amekabidhi vitabu hivyo kwa Jaji Mkuu wa Zanzibar
Omar Makungu ili vianze kutumika katika matumizi ya kila siku katika
hafla iliyofanyika ukumbi wa Mahakama kuu Vuga mjini Zanzibar.
Mkuu huyo wa Kitengo cha uandishi wa Sheria amesema kuwa Sheria hizo
zinahitaji umakini mkubwa kuweza kuzitumia hivyo ipo haja ya kutolewa
mafunzo kwa watakaotumia sheria hizo kutokana na utaratibu mpya
uliowekwa katika sheria hizo.
‘’Si rahisi kuwa kila mwanasheria anaweza kuzielewa sheria hizo
kwakuwa tu zimeandikwa katika vitabu, inahitaji umakini mkubwa kuweza
kuzielewa’’. Alisema Saleh .
Aidha amefahamisha kuwa sheria zilizofanyiwa marekebisho zitaweza pia
kupelekwa katika Ofisi za Muungano pamoja na tume za haki za binaadamu
nchini.
Hata hivyo amesema sheria hizo zimefanyiwa marekebisho makubwa
jambo ambalo limepelekea kuwa na vitabu vichache badala ya kuwa na
vitabu vingi ambavyo vilikuwa vikitumika hapo awali.
Mwanasheria huyo amesema Sheria hizo hazikuvunja historia
kilichofanyika ni kuondolewa kwa zile sheria zisizofanya kazi na
kuziacha zile zinazotumika kuweza kufanya kazi.
Sambamba na hayo ameleza kuwa Sheria hiyo imeweza kuandikwa kwa lugha
nyepesi tofauti na mwanzo ili kuweza kuwawezesha wasomaji kuelewa kwa
haraka .
Nae Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu amesema Vitabu hivyo
vitaisaidia sana Mahakama kuweza kufanya kazi zake kwa wepesi.
Amesema kuwa Vitabu hivyo pia vitaweza kuondoa changamoto kubwa kwa
Mahakama na kwamba maboresho zaidi yatakuja kadiri mahitaji
yatakapojitokeza.
Hata hivyo ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa
kuweza kuwakabidhi vitabu hivyo ambavyo vitaweza kusaidia katika
utekelezaji wa kazi zao.
chanzo: Zanzibar24.
Comments