
Meli hiyo kwa jina USS Michigan, ambayo ina uwezo wa
kushambulia kwa makombora, inatarajiwa kujiunga na kundi jingine la meli
za kivita zinazoelekea eneo hilo, zikiongozwa na meli kubwa ya kubeba
ndege ya Carl Vinson.
Korea Kaskazini inaadhimisha miaka 85 tangu kuanzishwa kwa jeshi lake Jumanne.
Miaka ya nyuma, imekuwa ikiadhimisha siku hiyo kwa kuzindua makombora na silaha nyingine.
Wasiwasi umeongezeka wiki za karibuni kutokana na Marekani na Korea Kaskazini kujibizana vikali na kutoleana vitisho.
Hayo
yakijiri, katika tukio ambalo si la kawaida, bunge lote la Seneti
nchini Marekani limealikwa kwa kikao cha kupashwa habari kuhusu Korea
Kaskazini siku ya Jumatano katika ikulu ya White House.
Nyambizi
ya USS Michigan hutumia nguvu za nyuklia na hubeba makombora aina ya 154
Tomahawk na wanajeshi 60 pamoja na meli nyambizi nyingine ndogo, gazeti
la Korea Kusini la Chosun Ilbo limeripoti.
Meli hiyo inatarajiwa
kushiriki kwenye mazoezi ya kijeshi pamoja na kundi la meli
zinazoongozwa na Carl Vinson, kundi ambalo lilitumwa eneo la Korea
kuonyesha ubabe wa kijeshi wa Marekani.
Meli hizo za kivita wakati mmoja zilizua utata baada ya suitafahamu kuhusu iwapo zilikuwa hasa zinaenelekea eneo la Korea.
Lakini maafisa wa jeshi la wanamaji la Marekani kwa sasa wamesema zinaelekea eneo hilo kama ilivyoamrishwa.
USS Carl Vinson mwanzoni ilikamilisha mazoezi na jeshi la
Australia na kisha kuondoka ikidhaniwa kwamba ilikuwa inaelekea pwani ya
Korea.
Lakini meli hiyo na meli nyingine zilipita na kuelekea upande wa Bahari ya Hindi.
Pyongyang ilikerwa sana na kutumwa kwa meli hiyo na
imetishia kuizamisha kwa "shambulio moja kubwa" dhidi ya ilichosema ni
uchokozi wa Marekani.
Rais wa Marekani Donald Trump alisema mapema
mwezi huu kwenye mahojiano ya runinga kwamba angetuma "kundi kubwa la
meli zenye nguvu" na kwamba Marekani ina nyambizi ambazo "zina nguvu
zaidi, nguvu zaidi kabisa kushinda meli hiyo (Carl Vinson) ya kubeba
ndege".
China imeendelea kuhimiza kuwepo kwa utulivu.
Rais Xi
Jinping, akizungumza kwa simu na Bw Trump mnamo Jumanne, alizihimiza
pande zote "kuvumiliana na kujiepusha na vitendo ambavyo vinaweza
vikaongeza wasiwasi zaidi".
chanzo:Bbc.
Comments