Kutokana na hilo, Spika Ndugai amesema Katibu wa Bunge ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi huo, atakiarifu Chadema siku mpya ya uchaguzi na endapo hakitawasilisha majina kwa kufuata kanuni, atatoa uamuzi mwingine.
Spika Ndugai aliyasema hayo bungeni wakati akijibu mwongozo wa Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) aliyetaka kufahamu msimamo wa Spika kuhusu msimamo unaoendelea kushikiliwa na Chadema kuhusu uchaguzi huo.
“Hadi sasa nafasi hizo mbili katika uchaguzi huu bado ni za Chadema. Katibu ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi atawaarifu ni lini sasa uchaguzi utafanyika.
“Ikumbukwe, uamuzi wa kusema wabunge hawa wawili watoke Chadema na mmoja atoke CUF ni uamuzi wangu mimi kama Spika. Zamani wakati wa Bunge la Mama Makinda (Anne) na Bunge la Sitta (Samuel) utaratibu haukuwa hivyo.
Wakati ule wagombea walipangwa katika kundi moja tu la kutoka upinzani na sio kama nilivyogawanya mimi,” alieleza Spika Ndugai na kuongeza: “Kwa hiyo kama itafika siku hiyo wasilete majina yanayotakiwa kikanuni, mimi huyu huyu ambaye niliamua vile, mimi huyu huyu nitaangalia upya uamuzi wangu.
Haiwezekani kukubali nchi itekwe kwa sababu tu Chadema hawajaleta majina ya wagombea wao ili tuweze kuwachagua wawili wenye sifa kuungana na wenzao ambao tayari wamepatikana.”
Chadema kupitia kwa Mwenyekiti wake wa Taifa, Freeman Mbowe imeendelea kushikilia msimamo wake kuwa chama hicho kitarejesha majina yale yale mawili ya Lawrence Masha na Ezekiah Wenje kama wagombea wake Bunge itakapohitaji majina mengine.
Katika hatua nyingine, Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) umelipongeza Bunge kwa kusimamia demokrasia na kutokubali kuyumbishwa na Chadema wakati wa uchaguzi wa wagombea wa EALA.
Katibu Mkuu wa UWT Taifa, Amina Makilagi aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana kuwa kitendo kilichofanywa na Chadema cha kuwasilisha wagombea wawili tena bila kuzingatia jinsia ni kitendo ambacho kinarudisha nyuma ukombozi kwa wanawake.
Nao upande mmojawapo wa Chama cha Wananchi (CUF) ulioshiriki uchaguzi huo umesema utakwenda mahakamani kupinga uendeshaji wa uchaguzi huo kwa madai kuwa uliendeshwa kwa hila kwa manufaa ya CCM na Serikali.
Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya CUF inayomtambua Katibu Mkuu Maalim Shariff Hamad, Ahmed Katani alidai chama hicho kimehujumiwa baada ya Bunge kumchagua Habib Mohammed Mnyaa ambaye jina lake liliwasilishwa na Kaimu Katibu Mkuu asiyetambuliwa na chama hicho, Magdalena Sakaya.
chanzo:Habarileo.
Comments