Mshitakiwa wa kesi ‘Malkia wa Pembe za Ndovu’ adai aliteswa.

MSHITAKIWA wa pili katika kesi ya kujihusisha na biashara ya meno ya tembo, Manase Philemon ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa alitoa maelezo huku akiteswa na kutishwa.

Philemon alidai hayo wakati wakiongozwa na Wakili wake, Nehemiah Nkoko mbele ya Hakimu Mkazi, Huruma Shaidi, kujitetea katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi inayomkabili pamoja na, raia wa China ‘Malkia wa Pembe za Ndovu’, Yang Feng Glan (66) na Salvius Matembo.

Philemon alidai kuwa Aprili 20,2014 alikamatwa maeneo ya Njia Panda ya Segerea wakati akienda kununua vinywaji kwa ajili ya biashara yake ya Motel. 


Alidai kuwa baada ya kukamatwa alipelekwa Kituo cha Polisi Stakishari na kuchukuliwa na askari polisi, Sajenti Beatus na kupelekwa Kituo cha Polisi Oysterbay ambapo askari huyo aliwataka vijana wawili waandae mazingira ya kumning’iniza mshitakiwa huyo kama popo.

Aliieleza mahakama kuwa alimhoji Beatus ni kwanini ameanza vitisho ambapo askari huyo alianza kumuandikia maelezo yake ikiwemo biashara yake ya ufugaji, kilimo, moteli na madini ya ng’ombe. 

‘’Afande Beatus nilimkabidhi simu mbili na Sh milioni 2.6 kisha aliagiza vijana wale wawili waje ambapo walikuwa na bomba, wakanifunga pingu miguuni na mikononi kunifunga pamoja miguu na mikono kwa kutumia bomba na kunifunga bandeji mdomoni ambapo nilining’inizwa kwenye meza kama popo miguu juu kichwa chini na kunipiga kwa kutumia rungu kwa saa 3,’’ alidai Philemon.

Mshitakiwa huyo alidai kuwa baadaye alifunguliwa pingu na kuulizwa kama yupo tayari kuendelea kutoa maelezo yake ambapo alimwambia kuwa ana hali mbaya kwa kuwa anajisikia kizunguzungu. Pia alidai kuwa Beatusi alimchukua na kumpeleka polisi Kijitonyama ambapo aliwekwa rumande. 

Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 5, mwaka huu kwa ajili ya kutoa uamuzi wa kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi kama mshitakiwa huyo aliteswa ama la.

Kesi hiyo ndogo ndani ya kesi ya msingi imeanza kusikilizwa baada ya Wakili wa upande wa utetezi, Jeremiah Mtobesya kupinga maelezo ya onyo ya Manase yasipokelewe kama kielelezo cha kesi hiyo mahakamani kwa sababu aliyatoa polisi na yalichukuliwa nje ya muda na alipigwa na kunyanyaswa. 

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22, 2014 kwa makusudi raia wa China, Yang Feng Glan aliongoza na kufadhili vitendo vya kijinai kwa kukusanya na kusafirisha vipande hivyo 706 vya meno ya tembo bila ya kuwa na kibali chochote kile kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori. 

Kwa upande wa washtakiwa Salvius na Manase wanadaiwa kuongoza makosa ya uhujumu uchumi kwa kusaidia biashara ya nyara za serikali kwa kukusanya, kusafirisha na kuuza meno ya tembo kwa nia ya kujipatia faida.
chanzo:Habarileo.

Comments