Ngaraba alidai hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Huruma Shaidi katika kesi
ya meno ya tembo ya Sh bilioni 5.4 inayomkabili Philemon, raia wa China,
Yang Feng Glan (66) maarufu kama ‘’Malkia wa Pembe za Ndovu’’ na
mfanyabiashara Salvius Matembo.
Awali, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alidai kuwa kesi hiyo
imekuja kwa ajili ya kusikiliza kesi ndogo ndani ya kesi kubwa baada ya
mshitakiwa Philemon kudai aliteswa na kupigwa wakati akichukuliwa
maelezo.
Shahidi huyo alidai Aprili 20, 2014 kati ya saa 9 na saa 12 jioni
alikuwa kituoni, na askari Beatus aliingia akiwa na mtu mmoja na kuingia
katika Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi.
Alidai kuwa baadaye (Beatus) alimwambia amuweke mtuhumiwa mahabusu
hadi upelelezi utakapokamilika, lakini mshitakiwa huyo alimwambia
amuandikie maelezo kabla ya kuingia mahabusu.
Akiongozwa na Wakili Nchimbi, shahidi alidai kuwa saa 11:30 jioni,
Beatus alimkabidhi mshitakiwa na kumueleza kuwa akae mahabusu kwa
kujihusisha na biashara ya ujangili wa meno ya tembo.
Alidai kuwa kabla ya kumuingiza kwenye kitabu cha usajili namba 5 cha
mwaka 2014, kwa ajili ya kumuweka mahabusu, Mkuu wa Upelelezi alimpa
Ripoti ya Polisi (RB) na kumueleza kuwa Makao Makuu ya Polisi imeagiza
mshitakiwa awekwe mahabusu kituoni hapo.
Aliendelea kudai kuwa alimsajili Philemon kwa namba 2033/2014 ambapo
mshitakiwa alimwambia kuwa yeye ni mfanyabiashara na mkazi wa Ukonga.
Aliendelea kudai kuwa, utaratibu wao hawamuingizi mtuhumiwa mahabusu
akiwa na matatizo ya kiafya na akikutwa nayo, anaenda kwa Mkuu wa Kituo
au ofisa yeyote kwa ajili ya kupata maelekezo ikiwa ni pamoja na
kupelekwa hospitali na endapo atalazwa atatakiwa kulindwa na kisha
anatakiwa kurudi na vyeti kutoka hospitalini.
Aliieleza mahakama kuwa saa 12:40 mshitakiwa aliingia mahabusu na
kwamba alikula na taarifa zake za afya alirekodi kuwa nzuri katika
kitabu hicho.
chanzo:Habarileo.
Comments