Uhusiano wa pande mbili wa Morocco na Rwanda unatazamiwa kuimarika baada ya serikali ya Rabat kufungua rasmi ubalozi wake mjini Kigali.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi huo hapo jana, Louise Mushikiwabo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda alisema ingawaje uhusiano wa nchi mbili hizo umekuwa mzuri hata kabla ya kufunguliwa ubalozi huo, lakini unatazamiwa kuimarika zaidi haswa katika uga wa kidiplomasia.
Ubalozi huo wa Morocco mjini Kigali ulianza shughuli zake mapema Februari mwaka huu, lakini kuzinduliwa rasmi kwake hapo jana kunaonekana kuwa hatua muhimu ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa nchi mbili hizo.
Youssef Imani, Balozi wa Morocco mjini Kigali kwa upande wake amesema: "Uzinduzi huu ni wa kimaonyesho na kidiplomasia tu, lakini kuna mengi yanafanyika kuhakikisha kuwa uhusiano wa pande mbili unaimarika zaidi."
Oktoba mwaka jana, Rwanda na Morocco zilitiliana saini mikataba 19 ya maelewano, juu ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyuga mbalimbali ukiwemo wa kibiashara.
Makubaliano hayo yalisainiwa baada ya Rais Paul Kagame wa Rwanda kuitembelea Morocco mwaka jana, huku Mfalme Mohammed VI wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika akiitembelea Kigali miezi minne baadaye.
chanzo:parstoday.
Comments