Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa UVCCM tawi la Mitandaoni Taifa, Mohammed Mchekwa ambaye ni mkulima wilayani Malinyi alipokuwa akizungumzia utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyopewa kipaumbele na mkurugenzi huyo katika halmashauri yake.
“Tunampongeza kwa dhati Mkurugenzi (Ndimbwa) kwani ni kutokana na ushauri wake vijana tumekuwa wakulima, tunakula kutokana na kile tulichopanda na kuvuna katika skimu za umwagiliaji ndani ya halmashauri yake.
“Ni jitihada zake zimetupa ujasiri wa kutembea kifua mbele huku mifuko yetu ikiwa imetuna fedha zitokanazo na mauzo ya mazao ya kilimo tuliyofanya wilayani Malinyi. Sasa tunajivunia ajira mpya kama wakulima ambao tunalima kwa msimu wote wa mwaka wala hatuhofii jua.
Skimu za umwagiliaji zinafanya kilimo chetu kuwa cha kisasa sana,”alisema. Halmashauri ya Malinyi imekuwa ikitiliza mkazo kilimo chenye tija kwa vijana, ambapo kupitia programu hiyo, Ndimbwa na Mbunge wa Jimbo la Ulanga Magharibi, Profesa Haji Mponda wameasisi kilimo cha mazao ya biashara ya korosho na kakao ili kuiandaa wilaya hiyo kuwa chachu ya uhamasishaji wa ujenzi wa uchumi wa viwanda kupitia uzalishaji wa malighafi za viwandani.
Kwa pamoja Mkurugenzi Ndimbwa na Mbunge Mponda kupitia program hiyo maalum wameziingiza katika mpango wa uzalishaji wa mazao ya biashara ya kakao na mkonge shule zote za msingi na sekondari wilayani humo ambapo kila shule ya sekondari kuanzia msimu huu wa kilimo italazimika kulima ekari tano za mazao hayo, huku kila shule ya msingi ikiagizwa kulima ekari mbili za mazao hayo.
Tayari Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mussa Iyombe ametoa baraka katika utekelezaji wa mpango huo ambao pamoja na kuchochea uzalishaji wa mazao hayo ya viwandani pia utaweza kuzijengea uwezo shule hizo na kuzifanya kujitegemea kwa chakula na ujenzi wa miundombinu ikiwemo mabweni kwa wanafunzi.
Mbali ya mkakati huo kuzihusi-sha shule, Mkurugenzi na Mbunge huyo wameazimia mpango huo kuvihusisha pia vijiji vyote vya Malinyi hatua ambayo itaiwezesha wilaya hiyo kuwa gwiji katika kilimo cha kakao na mkonge na hivyo kuiondoa katika kutegemea zao moja la mpunga kama ilivyozoeleka mwaka na mwaka.
chanzo:Habarileo.
Comments