MKE wa Rais wa Zanzibar,Mama Mwanamwema Shein, amesema serikali itaendelea kusimamia sera yake ya kutoa elimu bure, kwa wananchi wa Zanzibar.

Mama Shein, aliyasema hayo wakati akiwahutubia wananchi katika
sherehe ya kuwakabidhi vifaa mbali mbali kwa ajili wanafunzi wa Dahalia
ya skuli ya sekondari
ya Mohamed Juma Pindua Wilaya ya Mkoani Kisiwani
Pemba, ambapo amewapatia Mashuka, Mablangeti, Sabuni za kufulia na
kuogea.
Mama Shein, amesema kuwa serikali kutokana na kujali wananchi wake
hivi sasa imeamua kutoa elimu bure kwa ngazi ya msingi na sekondari,
jambo ambalo limefanywa kwa makusudi ili kuhakikisha kila Mzanzibari
anapata elimu .
Kutokana na hali hiyo, Mama Shein alisema ni vyema kwa Wazanzibari
hasa wazazi kuhakikisha wanatumia fursa hiyo kwa kusimamia elimu ya
Watoto wao ikiwa ni hatua itayowawezesha kuitikia wito wa serikali
unaowataka kila mtoto alietimiza umri anapatiwa elimu.
“Mheshimiwa Rais alifanya uamuzi wa kuondoa michango kwa wazee kwa ajili ya watoto wetu wanaosoma skuli za msingi, na vile vile serikali yetu imeamua kulipia gharama za mitihani kwa wanafunzi wa kidato cha pili cha nne na sita hatua zote hizo zinalengo la kumuondolea mzigo sisi wazazi wa kugharamia elimu kwa dhamira ile ile ya Muasisis wa Mapinduzi yetu Marehemu Mzee Abeid Amani Karume aliyoitoa Septemba 23 1964 ya kutangaza elimu bure” Alisema Mama Shein.
Alisema ili kuweza kupatikana kwa matunda hayo ni vyema kwa wazazi
kuhakikisha wanawasomesha watoto kwa bidii na sio kuwaacha watoroke
skuli kwani vitendo hivyo vinaweza kuwaharibia maisha yao.
Nae Mke wa Makamu wa Pili wa Rais, Mama Asha Suleiman Iddi,
amewataka wanafunzi hao, kuhakikisha wanasoma kwa bidii, na kuacha
kuingia katika mivutano ya kisiasa kwani hivi sasa imeonekana kwa
asilimia kubwa kuichafua sekta ya elimu.
Alisema inasikitisha kuona hivi sasa sekta ya elimu hasa katika Vyuo
vikuu kutumiwa na Wanasiasa kwa malengo ya kukuza mivutano jambo ambalo
tayari limeanza kuonyesha athari yake kwa walimu kushindwa kutimiza
wajibu wao wa kutoa elimu na badala yake wamekuwa wakiwaharibu
wanafunzi.
Alisema baya zaidi, walimu hao wamekuwa wakitumia nafasi zao vibaya
kwa kuwafelisha wanafunzi wanaowaona hawakubaliani na misimamo yao,
jambo ambalo ni hatari kwa mustakbali wa sekta ya elimu hapa Zanzibar.
Kutokana na hali hiyo, Mama asha,ameutaka uongozi wa Wizara ya Elimu
kuiona hali hiyo na kuhakikisha wanapiga vita vitendo hivyo, ili kuona
kila mwenye haki ya kupata elimu anatumia fursa hiyo, kama
ilivyokusudiwa na Mzee Abeid Amani Karume.
Mapema Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mmanga Mjengo
Mjawiri, akitoa maelezo yake, alisema ni kweli kumekuwa na hali hiyo na
tayari Wizara ya Elimu inakusudia kutoa adhabu kwa wahusika wote baada
ya kubaini kuwapo kwa kasoro kadhaa ndani ya sekta hiyo likiwemo suala
la siasa katika skuli.
Nae Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo, akitoa maelezo yake, alisema tangu
waingie katika kituo hicho wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la uhaba wa
huduma ya maji safi na salama na ameiomba serikali kuliangalia suala
hilo.
Hata hivyo aliipongeza serikali kwa jitihada ilizozifanya za
kuhakikisha inajenga kituo hicho ambacho hivi sasa kimechangia kwa kiasi
kikubwa kuinua sekta ya elimu hapa Kisiwani Pemba.
chanzo:zanzibar24.
Comments