
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein Aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na
mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya ‘Engineering Consultants Group’
Mhandisi Amr Hassan Allouba, Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake, Dk. Shein aliyasema kuwa
katika kuimarisha utekelezaji wa Mipango miji, Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar imo katika jitihada za makusudi za kuhakikisha inashirikiana
na Kampuni mbali mbali za ndani na nje ya nchi katika ujenzi wa miji ya
kisasa hapa Zanzibar.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa azma ya Serikali ni kuufanya Mji wa
Zanzibar kupiga hatua kubwa zaidi za kimaendeleo katika maamuzi ya
ziada ya kufanya kitovu cha Mji (Ngambo) kuwa ni ‘Smart City’ ambayo ni
nadharia mpya yenye lengo la kufanya miji iwe sio tu mizuri ya kileo na
endelevu bali hutumia utaalamu na teknolojia mpya.
Dk. Shein alisema kuwa kujitokeza kwa Kampuni hiyo na kuonesha azma
ya kutaka kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika sekta
hiyo ni jambo la faraja hali ambayo inatoa nafasi kwa Zanzibar kuzidi
kujiwekea mazingira mazuri katika utekelezaji wa azma hiyo sambamba na
kujipanga vyema kiuwekezaji.
Rais Dk. Shein alimueleza Mwenyekiti huyo wa Kampuni ya ECG yenye
Makao Makuu yake mjini Cairo, Misri kuwa tayari Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar imeshatenga maeneo huru ya uwekezaji Fumba kwa upande wa
Unguja na Micheweni kwa upande wa Pemba na katika maeneo yote hayo
Serikali inaendelea kutoa fursa kwa wawekezaji kuekeza katika sekta
mbali mbali za maendeleo.
Aliongeza kuwa Zanzibar iko tayari kushirikiana na Kampuni hiyo kwani
itapata mengi ya kujifunza kutokana na uzoefu mkubwa ulionao na
kusisitiza kuwa ujenzi wa miji mipya ya kisasa inahitajika hasa
ikizingatiwa kuwa maendeleo na teknolojia yamezidi kuimarika duniani
kote ambapo kampuni hiyo nayo iko katika hatua hiyo.
Aidha, Dk. Shein alimueleza Mwenyekiti huyo alieongozana na kiongozi
wa Kampuni hiyo kwa upande wa nchi za Bara la Afrika Sherif Mourad
wakiwa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri, Balozi
Mohammed Hamza kuwa Zanzibar ina uhusiano na ushirikiano mwema na
wakihistoria kati yake na Misri.
Aliongeza kuwa Misri ni miongoni mwa nchi za mwanzo zilizoanzisha
uhusiano wa kidiplomasia kati yake na Zanzibar mara tu baada ya
Mapinduzi Matkukufu ya Januari 12, 1964 hatua ambayo ilipelekea
mashirikiano mazuri yaliopelekea kukuza uhusiano na ushirikiana katika
sekta ya elimu, afya na nyenginezo.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa wanafunzi walio wengi wa
Zanzibar walipata fursa ya kusoma nchini Misri hasa katika Chuo Kikuu
cha Al-Azhar na vyuo vyenginevyo na wengine kupata fursa ya kusomea
udaktari na fani nyengine zikiwemo za elimu ya dini ya Kiislamu, habari
na nyenginezo.
Nae Mwenyekiti wa Kampuni ya ‘Engineering Consultants Group’ Mhandisi
Amr Hassan Allouba alimueleza Dk. Shein azma ya Kampuni hiyo
kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha miji mipya ya kisasa ambayo
inaendana na teknolojia ya kisasa ambayo itaiwezesha Zanzibar kuimarika
kiuchumi, kibiashara na utoaji huduma kwa jamii.
Mhandisi Allouba alimuelezea Dk. Shein uzoefu wa kazi za Kampuni hiyo
ndani na nje ya Misri pamoja na mafanikio iliyoyapata na kueleza kuwa
Kamupuni yake iko tayari kuleta neema hiyo kwa Zanzibar ili kuwasaidia
wananchi pamoja na Serikali yao katika kukuza uchumi wake na kuimarisha
maendeleo.
Alieleza kuwa miradi hiyo kwa uzoefu wake imekuwa ni kichocheo
kikubwa cha ajira hali ambayo imepelekea kuimarika kwa soko la ajira
katika maeneo yote ambayo tayari wameshaitekeleza.
Alisema kuwa mbali ya kuimarika kwa ajira pia, hatua hiyo itasaidia
katika kuifanya Zanzibar iimarike na iwe mbele katika sekta ya
teknolojia ya kisasa kutokana na uzoefu walionao katika miradi hiyo.
Hivyo, Mwenyekiti huyo amemuhakikishia Dk. Shein kuwa Kampuni yake
iko tayari kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Misri na
Zanzibar kwa kuja kuekeza Zanzibar kwani ni pande mbili zenye uhusiano
na udugu wa kihistoria, hivyo hatua hiyo itapanua wigo wa maendeleo kwa
Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
chanzo: zanzibar24.
Comments