Miliki za NSSF zafanyiwa ukaguzi maalumu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenista MhagamaSERIKALI imefanya ukaguzi maalumu wa miliki za Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kupitia utendaji na uwekezaji kwenye majengo, mashamba na viwanja vyote vinavyomilikiwa na mfuko huo, imeelezwa.

Hatua hiyo inatokana na hoja ya mwaka wa fedha 2016/17 ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria iliyoiagiza wizara katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu kuifanyia kazi ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kamati hiyo iliagiza hayo ili kubaini ukweli kuhusu tuhuma za ubadhirifu wa fedha katika miradi ya NSSF na kuwachukulia hatua kali za kisheria, kiutaratibu na kinidhamu wote watakaoonekana kuhusika na ubadhirifu wa fedha hizo za umma na wanachama wa mfuko huo.
Akifafanua utekelezaji wa hoja hiyo, mbele ya kamati hiyo hivi karibuni, Waziri Jenista Mhagama alisema, Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kwa kushirikiana na Benki Kuu (BoT), ilifanya ukaguzi wa miliki za NSSF kwa mwaka wa fedha 2016/17.
“Taasisi hizo zilipitia kwa kina utendaji na uwekezaji kwenye majengo, mashamba na iwanja vyote vinavyomilikiwa na mfuko. Ukaguzi huo ulibainisha mapungufu mengi katika uwekezaji wa wa miliki za mfuko ikiwamo malimbikizo ya kodi za pango,” alisema Mhagama.
Alifafanua kuwa pia ukaguzi huo ulibaini ukosefu wa hati miliki kwa baadhi ya mejengo na viwanja, ununuzi wa bei kubwa kwa baadhi ya viwanja, utata katika ununuzi wa baadhi ya viwanja na ujenzi usiokuwa na upembuzi yakinifu.
Kwa mujibu wa Mhagama, Bodi imewasimamisha kazi baadhi ya maofisa kuwezesha uchunguzi wa kina kufanyika na imeidhinisha kusimamishwa uendelezaji wa baadhi ya miradi wakati uchunguzi ukiendelea.
chanzo:Habarileo.

Comments