Siku
moja baada ya kutokea kwa vurugu kubwa katika mkutano wa viongozi wa
Chama cha Wananchi (CUF) Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam kwa kuvamiwa
na genge la watu waliokuwa na silaha za moto, wabunge wa upinzani
wameibuka na kuitupia lawama Serikali.
Kutokana
na hali hiyo wabunge hao wamesema ukimya wa Serikali kuhusu uvamizi huo
wa viongozi wa CUF, huku wakitangaza kumwandikia barua Mkuu wa Jeshi la
Polisi (IGP), Ernest Mangu pamoja na taasisi nyingine za Serikali
kuhusu tukio hilo.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini Dodoma, Naibu Mnadhimu wa Kambi rasmi ya
Upinzani bungeni, Ally Saleh alishangazwa na ukimya wa Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe kwa kushindwa
kujitokeza na kukemea hatua ya waandishi wa habari kupigwa katika
mkutano huo.
Kutokana
na hilo, wamelaani kitendo hicho cha uvamizi wa mkutano pamoja na
waandishi wa habari kupigwa huku wakiitaka Serikali kutoa tamko na
kuchukua hatua kali dhidi ya waliohusika.
Wakati wabunge hao wakitoa tamko hilo, Dk. Mwakyembe yeye amekana kuwa taarifa juu ya tukio hilo.
“Mimi
sijui chochote ndiyo nasikia kwako, kwani hao wabunge wamekwambia kama
wameniletea taarifa hizo? Mimi niko Dodoma…sifahamu chochote,” alisema.
Akizungumzia
hali hiyo Saleh, alisema chama cha CUF, kimeshamwandikia barua IGP
Mangu pamoja na taasisi nyingine za Serikali kuhusu tukio hilo.
Alisema
ukimya wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba na Dk. Mwakyembe
juu ya tukio hilo umeonesha kuwa hawajatimizi majukumu yao ipasavyo.
“Mambo haya yanavyotokea mawaziri wawili tunataka kuwavisha mnyororo, Waziri Mwigulu Nchemba na Mwakyembe.
“Mwakyembe
alipaswa kujitokeza kwa haraka na kutoa tamko, tunahisi jukumu la
Serikali halijatekelezwa, Mwakyembe anapaswa kuhakikisha usalama wa
waandishi unakuwapo,” alisema.
Saleh
ambaye ni Mbunge wa Malindi alisema kikundi cha ‘Mungiki’ si kigeni
hapa nchini na Serikali inakifahamu lakini hakuna hatua zozote ambazo
zimeshachukuliwa hadi sasa.
Aidha
alisema kutokana na tukio lililotokea juzi, ziara iliyokuwa ifanywe na
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad upande wa bara jana
ilifutwa na Serikali.
“Kitendo
cha Serikali kuufuta mkutano huo si sawa kwa sababu bwana yule (Profesa
Ibrahim Lipumba) anabebwa na mbereko ya Serikali kwa kufanya mikutano
ya ndani kila wakati.
“Serikali
inalea Jamhuri ndogo ndani ya Jamhuri, vile vile Serikali imekuwa
inalea kambi ndogo ndani ya Buguruni na kwamba wanufaika zaidi wa
mgogoro unaoendelea ndani ya CUF ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao
dhumuni lao ni kuchukua majimbo yanayoongozwa na CUF katika uchaguzi
mkuu ujao,”alisema.
Kwa
upande wake Naibu Waziri Kivuli wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Devotha Minja alisema matukio wanayofanyiwa waandishi wa
habari yanapaswa kukemewa.
“Waandishi
wa habari ni kiungo cha serikali na wananchi, pia ni kiungo kati ya
wanasiasa na wananchi, suala walilofanyiwa jana linapaswa kukemewa na
halipaswi kuendelea kutokea,” alisema Minja.
Minja
ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), alisema waandishi wa
habari wamekuwa wakionewa na kupigwa, akitolea mfano wa tukio la
kuvamiwa kwa Kituo cha Televisheni cha Clouds, kutekwa na kuteswa kwa
Absalom Kibanda, kuuawa kwa aliyekuwa mwandishi wa Channel Ten, Daud
Mwangosi.
Kutokana
na vurugu hizo ambazo zilisababisha mtu mmija anayedaiwa kuvamia
mkutano huo kujeruhiwa, Jeshi la Polisi limesema bado linaendelea na
uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo na hadi sasa hakuna mtu yeyote
anayeshikilia.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Suzan Kaganda, amesema bado
wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ikiwa ni pamoja na wahusika
waliosababisha vurugu hizo.
“
Kwa sasa hatuwezi kuzungumzia jambo lolote kuhusu tukio
hilo…tunaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu vurugu hizo na baada ya
uchunguzi wetu kukamilika tutatoa taarifa ,”alisema Suzan.
chanzo:mpekuziblog.
Comments