Akijibu mwongozo huo, Dk Tulia amesema Bunge haliwezi kutoa msimamo
wa suala hilo kwa vile pamoja na kuwa zipo biashara zinazofungwa kwa
ugumu wa mazingira ya kufanya biashara, lakini zipo pia zinazoanzishwa.
Awali akiomba mwongozo huo, Mwakajoka alisema; “Mheshimiwa Naibu
Spika zipo taarifa kwamba wafanyabiashara wanafunga maduka yao, mahoteli
yao.
“Hatua hii mheshimiwa Naibu Spika inasababisha serikali ipoteze
mapato mengi ambayo yangetokana na kodi kama biashara hizi zingeendelea
kuwepo na hadi sasa hakuna utatuzi wowote wa jambo hili. Nataka tu
kufahamu katika hili, Bunge linaweza kuchukua hatua gani ili kuweza
kuisimamia serikali iweze kurekebisha hali hiyo?”
Naibu Spika akijibu alisema pamoja na kuwa mbunge huyo ameomba
mwongozo huo kinyume cha utaratibu kutokana na Kanuni kusema wabunge
wataomba mwongozo kutokana na jambo lililotokea mapema bungeni, lakini
suala hilo limewahi kutolewa majibu bungeni.
"Waheshimiwa wabunge suala hili halipo kabisa katika shughuli za leo
hata katika maswali yaliyoulizwa leo hakuna mahali suala hili
limejitokeza. Kwa hiyo si la mapema leo.
"Lakini niseme wazi kama ambavyo Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
amewahi kusema hapa bungeni siku zilizopita, wakati zipo biashara
zinafungwa lakini zipo zinazofunguliwa pia," alisema Naibu Spika.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Buyungu, Samson Bilago (Chadema)
aliomba mwongozo kwa Spika akitaka kufahamu ni kwa nini Bunge
halikumchukulia hatua Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga aliyetumia lugha
ya kuudhi wakati akichangia bungeni.
Akitumia Kanuni ya 64 (1) vipengele vidogo vya (f) na (g), Mbunge
huyo alisema Mlinga akichangia bungeni alisema alishindwa kufahamu ni
nani alikuwa mgombea mwanamke kwa kiti cha Bunge la Afrika Mashariki
(EALA) kutoka Chadema kati ya Lawrence Masha na Ezekia Wenje.
Bilago alisema hatua ya mbunge huyo kutoa matamshi hayo ya kuudhi
bila Bunge kumchukulia hatua ilikuwa ni sawa na kuwalinda wabunge wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) huku wabunge wa upinzani wakishughulikiwa.
Hata hivyo, Naibu Spika alisema asingeweza kutolea mwongozo suala
hilo kwa vile si jambo la mapema na kuwa hata siku Mlinga alipotoa
maneno hayo hakuwepo katika kiti cha Spika.
chanzo:Habarileo.
Comments