Umbula alitaka kujua wilaya na vijiji vinavyoongoza kwa mila potofu
ya ukeketaji wanawake kama ulivyooneshwa katika takwimu za utafiti
uliofanywa mwaka 2010 na kubaini mkoa wa Manyara ndio kinara wa
ukeketaji nchini. Alitaja pia kujua athari na idadi ya vifo mkoani
Manyara, lakini pia mkakati wa dharura wa kukabiliana na mila hiyo
potofu ili kuondoa kabisa athari za ukeketaji.
Akijibu, Kigwangalla alisema katika utafiti huo, ni kweli Manyara
ilibainika kuwa na ukeketaji kwa asilimia 100 hasa maeneo ya vijijini na
kuongeza kuwa, wilaya zote za mkoa wa Manyara zinajihusisha na vitendo
hivyo, hasa wilaya ya Hanang. Aliyataja makabila yanayofanya ukeketaji
katika wilaya hiyo kuwa ni Wairaki, Wabarbaig na Wanyaturu, wengi wakiwa
katika maeneo ya Kata za Balanglalu na Basutu.
Akizungumzia athari, alisema ni kubwa sana kwa wanawake hasa wakati
wa kujifungua, kwani huweza kusababisha ulemavu wa kudumu, vifo kutokana
na kutokwa na damu nyingi, maumivu makali, kupatwa ugonjwa wa fistula
na wakati mwingine kupata madhara ya kisaikolojia. Alisema ni vigumu
kutambua vifo vinavyotokana na ukeketaji, kwani hufanyika kwa siri
katika jamii hiyo. Kuhusu kukabiliana na tatizo hilo, alisema Serikali
imetunga sheria mbalimbali.
Hata hivyo, alisema sheria pekee bila elimu kwa umma haiwezi kumaliza
tatizo hilo.
Aliongeza kuwa, kwa sasa wanatumia zaidi maofisa maendeleo
wa ustawi wa jamii ili kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi
kuondokana na mila na tamaduni hizo. Aliwataka pia wabunge na viongozi
mbalimbali kushiriki katika kuhamasisha wananchi kuondokana na mila
hizo.
chanzo:Habarileo.
Comments