Makamishna wa kodi EAC wakutana Dar.

Dickson KateshumbwaMAKAMISHNA wa Mamlaka za Kodi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana na kujadiliana namna ambavyo wanaweza kupunguza gharama za kufanya biashara katika ukanda huo.
Mwenyekiti wa mkutano huo, Kamishna wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Uganda (URA), Dickson Kateshumbwa alisema mkutano huo ambao uliwahusisha wataalamu wa kodi, makamishna wa forodha na makamishna wa mamlaka una lengo la kujadili namna gani Afrika Mashariki itaweka mazingira mazuri ya watu wake waweze kufanya biashara.

Alisema katika mkutano huo walijadiliana masuala yanayohusu himaya moja ya forodha, muunganiko wa huduma za kiforodha, mapitio ya viwango vya ushuru na kanuni za uasili wa bidhaa, utekelezaji wa vituo vya huduam ya pamoja mipakani, utekelezaji wa mradi wa huduma kwa wafanyabiashara wenye idhini maalumu.
Eneo lingine ambalo walijadiliana ni utekelezaji na kuidhinishwa kwa mtaala wa mafunzo ya forodha kwa nchi za Afrika Mashariki, makubaliano ya masuala ya kibiashara ya kidunia na kutengeneza mswada wa sheria ya usiamjmizi wa mawakala wa forodha.
Kateshumbwa alisema utekelezaji wa himaya moja ya forodha ambao ulianza 2014 katika korido ya kaskazini na kati, chini ya utaratibu huo bidhaa zinaangaliwa katika mpaka wa kwanza ambao bidhaa zimeingilia katika ukanda wa Afrika Mashariki na kuendelea upande wa nchi nyingine.
Alisema kodi na ushuru unalipwa hapo hapo. Aliongeza kuwa utaratibu huo umepunguza gharama za kufanya biashara ambapo muda wa kutoa mzigo mpakani umepungua kutoka wastani wa siku 21 mpaka siku 3 hadi tano.
“Ili kutekeleza mradi huu maofisa wa forodha wamepelekwa katika mipaka ya nchi wanachama na hii imesaidia kupunguza biashara za magendo mipakani,” alisema Kateshumbwa.
Alisema hadi sasa kuna bidhaa ambazo zimewekwa kwenye mpango huu kwa majaribu, lakini jambo muhimu lililoazimiwa katika mkutano ni kwamba ifikapo Juali 31 mwaka huu, bidhaa zote zitapita kwa utaratibu huu.
Pia alisema EAC pamoja na TRA wanaangalia uwezekano wa kuunganisha mfumo wa kufuatilia mzigo na ule wa kanda. Kuhusu muunganiko wa huduma za kiforodha, alisema mifumo ya forodha imeboreshwa ikiwemo Kenya (Icms), Tanzania (TANCis) na Uganda na Burundi (ASYCUDA world).
Eneo lingine ambalo makamishna hao walijadiliana ni mapitio ya viwango vya ushuru na kanuni za uasili wa bidhaa kutokana na mabadiliko ya mazingira ya biashara duniani. Alisema jumuiya inafanya mapitio ya viwango vya ushuru ili kuendana na hali halisi katika kipindi cha miaka mitano.
Alisema jumuiya ya Afrika mashariki imeridhia na inatekeleza makubaliano ya WTO kwa kurahisisha ufanyaji biashara ikiwemo nyaraka na taratibu na kiforodha. Lakini pia alisema wanaangalia uwezekano wa kutengeneza mswada wa sheria ya usimamizi wa mawakala wa forodha. Alisema eneo hilo linatekelezwa kwa kushirikisha sekta bianfsi na mamalak za mapato na shirika la amaendeleo la Japan (JICA).
chanzo:Habarileo.

Comments