Mahiga alipongeza baraza la usalama UN.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga.WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri ya Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dk Augustine Mahiga amelipongeza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kwa kuridhia na kupitisha Azimio Namba 2348 (2017) la kuiongezea muda Misheni ya Ulinzi wa Amani chini ya MONUSCO iliyopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hadi Machi 31 mwaka kesho.


Alitoa pongezi hizo wakati akihutubia baraza hilo kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani hivi karibuni.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Dar es Salaam na wizara hiyo, Balozi Mahiga aliyewakilisha nchi 15 za SADC, aliipongeza UN kwa ujumla chini ya uongozi wa Katibu Mkuu, Antonio Guterres kwa kuongeza muda kwa Monusco na jitihada nyingine nyingi za kutafuta suluhu ya kudumu kwa changamoto mbalimbali zinazoikabili DRC kwa muda mrefu ikiwemo ukosefu wa amani na usalama.

Alisema kupitishwa kwa azimio hilo kunatoa matumaini mapya kwa wananchi wa DRC na dunia kwa ujumla kwamba UN ina nia ya dhati kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana nchini humo.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuiomba UN kutambua mchango mkubwa unaotolewa na Kikosi Maalumu cha Force Brigade Intervention- FIB kilichoundwa na SADC ambacho kinashirikiana na Monusco katika ulinzi wa amani DRC.

FIB ina mchango wa vikosi vya ulinzi wa amani kutoka nchi tatu za SADC ambazo ni Tanzania, Afrika Kusini na Malawi.
chanzo:Habarileo.

Comments