Wiki moja iliyopita, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqqaro
alifanya ziara katika kata zote 25 za Jiji la Arusha ya kuangalia
shughuli za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya chini ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na kutatua kero za wananchi wa kata hizo.
Mbali ya mkuu wa wilaya kuwepo katika ziara hiyo, pia alikuwepo
Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia na wakuu wote wa
idara za jiji hilo, watendaji wa kata zote ikiwa ni kutaka kutatua kero
za hapo kwa hapo zitakazoulizwa na wananchi wa kata husika na kupatiwa
majibu.
Madiwani wa Chadema walioandikiwa barua na kutakiwa kujieleza kabla
ya kesho Aprili 26, mwaka huu ni Diwani wa Kata ya Kimandolu, Elishadai
Ngowi na Diwani wa Kata ya Terrat, Obeid Meng’oriki.
Nakala ya barua hiyo iliyoandikwa na Katibu wa Chadema Wilaya ya
Arusha, Stephen Urassa, imewataka madiwani hao kujieleza ni kwa nini
wameisifu Serikali ya Rais Magufuli katika mikutano ya hadhara ya Mkuu
wa Wilaya ya Arusha alipokuwa akifanya ziara katika jiji hilo.
Urassa
katika barua hiyo, alidai kuwa kufanya hivyo ni ukiukwaji wa kanuni na
taratibu za Chadema, hivyo ni kwa nini madiwani hao wasichukuliwe hatua
kwa uamuzi huo waliofanya unaodaiwa ni kinyume cha Katiba na kanuni za
chama.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Diwani wa Kimandolu,
Ngowi alikiri kupata barua hiyo na kusema atatimiza kile alichotakiwa
kueleza katika barua hiyo. Diwani Ngowi alisema hakuwa mnafiki kumsifu
Rais Magufuli hadharani katika mkutano wa hadhara wa mkuu wa wilaya
alipotembelea kata hiyo kwa kuwa anasifu kitu kilichofanywa katika kata
hiyo na nchi kwa ujumla.
Alisema anaamini kuwa Serikali ya Jiji la Arusha pamoja na uongozi wa
wilaya hiyo wakiongozwa na Kiranja Mkuu, Dk Magufuli wanafanya vema
katika kuboresha miundombinu ya Jiji la Arusha na kutatua kero za
wananchi, hivyo haoni kama ina tatizo lakini kuna baadhi ya watu ndani
ya chama hicho wanapotosha ukweli.
Diwani wa Kata ya Terrat, Meng’oriki
hakupatikana kwa njia ya simu kueleza kama amekubaliana na hatua ya
uongozi wa Chadema Wilaya ya Arusha kumwandikia barua hiyo kwa kosa la
kuisifu serikali, kwani simu yake iliita bila ya kupokelewa.
Hata hivyo, baadhi ya madiwani katika kikao cha Baraza la Madiwani
walijitokeza waziwazi kumsifu DED Kihamia kwa kazi nzuri anayofanya ya
kujenga miundombinu ya jiji hilo na kuwa lenye hadhi kubwa kiasi cha
kufananishwa na Geneva ya Afrika. Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa
madiwani hao ambaye aliomba kuhifadhiwa jina, alisema kumsifu mteule wa
Rais ni kuisifu serikali nzima ya Rais Magufuli na haoni sababu ya
madiwani wengine kutaka kuchukuliwa hatua.
Aliutaka uongozi wa Chadema Arusha kuacha kufanya siasa za maji taka
kwani siasa hizo zimepitwa na wakati na kumsifu mpinzani sio kosa, kwani
kuna baadhi ya viongozi wa juu wa Chadema wamekuwa wakiwasifu mawaziri
wa Serikali ya Awamu ya Nne na Tano hadharani, lakini hawachukuliani
hatua.
chanzo;HABARILEO.
Comments