Aidha, amepiga marufuku kuanzia leo usafirishaji wa mazao ya misitu
ndani na nje ya nchi kwa kutumia nakala zisizo halisi, kuunga mkono Sera
ya Uchumi wa viwanda ya Serikali ya Awamu ya Tano hakuna gogo
litakalosafirishwa kwenda nje ya nchi.
Amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa 24 wa Baraza la Wafanyakazi
wa Wizara ya Maliasili na Utalii, uliofanyika kwenye Ukumbi wa LAPF
mjini Dodoma na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali kutoka kwenye Idara,
Vitengo na Taasisi mbalimbali zilizopo chini ya wizara hiyo.
“Kuanzia mwezi Julai hakuna ruhusa ya kutoa vibali vya kuhamisha mkaa
kutoka wilaya moja kwenda wilaya nyingine, mkaa utachomwa, utauzwa
ndani ya wilaya kwa ajili ya matumizi ya Watanzania wanaohitaji nishati
ya mkaa, lakini biashara ya mkaa ya kutoa Dodoma kwenda Dar es Salaam
mpaka Zanzibar marufuku.
“Wamekata misitu yetu yote, mito yetu imekauka, tunashindwa kupata
maji ya umwagiliaji kwa sababu watu wengi huko nje wanataka mkaa wetu,
Tanzania jamani sio shamba la bibi, wale wote watakaotoa mkaa kutoka
eneo moja hadi jingine kinyume na sheria hii watashuulikiwa kwa
utaratibu wa uhujumu uchumi,” alisema Maghembe.
Alisema kwa upande wa miji mikubwa kama Dar es Salaam, Dodoma,
Morogoro na Tanga vitaanzishwa viwanda maalumu vya kuzalisha mkaa ambao
utauzwa kwa vibali maalumu katika mikoa mbalimbali nchini.
Alisema mkaa huo hautakuwa na athari nyingi za kimazingira kwa sababu utazingatia taratibu za uzalishaji endelevu.
Aidha, amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania (TFS) kumhamisha kituo cha kazi Mkuu wa Kikosi cha Kufuatilia
na Kuzuia Uharibifu wa Misitu, Arjason Mloge kutoka Makao Makuu ya TFS
kwenda Chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI) mkoani Kilimanjaro na badala
yake atafutwe mtu mwingine muaminifu.
Alisema uamuzi huo ni kufuatia udhaifu uliojitokeza katika
usafirishaji wa rasilimali za misitu ndani na nje ya nchi ikiwemo
usafirishaji kwa kutumia nakala za vibali ambazo sio halisi, yaani za
kudurufu.
“Agizo hili litekelezwe mara moja kabla ya saa sita mchana wa leo
(jana) na niwe nimepewa nakala ya barua hiyo ya uhamisho,” alieleza.
Kutokana na uamuzi huo, amepiga marufuku kuanzia leo usafirishaji wa
mazao ya misitu ndani na nje ya nchi kwa kutumia nakala zisizo halisi.
Ameongeza kuwa katika kuunga mkono Sera ya Uchumi wa Viwanda ya
Serikali ya Awamu ya Tano, hakuna gogo litakalosafirishwa kwenda nje ya
nchi.
“Wawekezaji wanahimizwa kujenga viwanda vya kuchakata magogo hayo
hapa nchini ili kutoa ajira kwa Watanzania pamoja na kutoa faida halisi
inayotokana na rasilimali hizo kwenye uchumi wa taifa,” alieleza waziri
huyo.
Akizungumzia changamoto ya mifugo kwenye maeneo ya hifadhi nchini,
alisema Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 sehemu
ya 21 (1) hairuhusiwi kabisha kuchunga mifugo katika Hifadhi za Taifa,
Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na Hifadhi za Misitu.
Amewataka watumishi wa Maliasili kusimamia sheria hiyo pamoja na kutoa mwito kwa wananchi kuifuata kikamilifu.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Aloyce Nzuki
alimueleza Waziri Maghembe kuwa maelekezo yote aliyoyatoa yamepokelewa
kwa ajili ya kuyafanyiwa kazi, huku Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya
Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa akimueleza waziri huyo kuwa
watalinda na kusimamia Maliasili za Taifa na kwamba katu hawapo tayari
kuandikwa kwenye vitabu kuwa walishiriki katika kutoweka kwa maliasili
hizo.
chanzo:Habarileo.
Comments