‘Kuwakosesha watoto chanjo nao ni ukatili’.

MKUU wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza amesema kuwakosesha watoto chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali ni aina mpya ya ukatili kwa watoto unaohatarisha maisha yao. Akizungumza katika Mtaa wa Msisina pembezoni mwa Manispaa ya Iringa jana wakati akizindua kimkoa Wiki ya Huduma za Chanjo mkoani Iringa, Masenza alisema, “Wazazi au walezi wanaozuia, au kupuuza na kuwakosesha watoto wao kupata huduma ya chanjo, wanafanya ukatili.”

Alisema takwimu za mwaka 2016 zinaonesha watoto 2,243 sawa na asilimia sita hawakukamilisha chanjo ya kuzuia magonjwa ya dondakoo, kifaduro, pepopunda, homa ya ini, homa ya uti wa mgongo na ugonjwa wa kupooza. Masenza alisema takwimu hizo zinaonesha watoto 1,495 sawa na asilimia nne hawakupata chanjo ya surua wakati watoto 5,979 sawa na asilimia 16 hawakupata dozi ya pili ya kukamilisha hiyo.


“Kwa takwimu hizi inaonesha watoto wengi hawakupata au kukamilisha chanjo zao kwa wakati na wapo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo,” alisema. 

Aliwataka wazazi na walezi wenye watoto wa miaka chini ya mitano kuitumia wiki hiyo kuwapeleka watoto wao katika vituo vya huduma ili wakapate huduma hiyo. Diwani Bashiri Mtove, alisema, “Kata hii ambayo ukubwa wake ni kilometa za mraba 162 ina zahanati moja tu na kwa mfano watu wa mtaa huu wa Msisina ili wafike katika zahanati hiyo wanahitaji kutembea zaidi ya kilometa 12.”

Masenza aliahidi kuchangia Sh milioni moja kwa masharti kwamba, lazima zahanati hiyo iwe na chumba maalumu kwa ajili ya huduma ya mama na mtoto. Mratibu wa Huduma za Chanjo Mkoa wa Iringa, Naftal Mwalongo alisema chanjo hizo zinatolewa ikiwa ni utekelezaji wa malengo endelevu ya dunia yanayohusu afya ili kupunguza vifo vya watoto wa miaka mitano ifikapo mwaka 2020.
chanzo:Habarileo.

Comments