Kuendelea ukosoaji kuhusu mapatano yaliyofikiwa kati ya Italia na Libya kuhusu wakimbizi.


Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka imezitaja taathira hasi za mapatano yaliyofikiwa kati ya Italia na Libya ili kuwazuia wahajiri kuelekea Ulaya kuwa ni hatari na zisizo na kibinadamu.


Mkurugenzi wa Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) amesema makubaliano yaliyofikiwa kati ya Italia na serikali ya Libya huko Tripoli, inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kwa lengo la kuwahifadhi wahajiri kwa njia ya kibinadamu katika ardhi ya Libya, hayawezekani kutekelezeka. 

Italia na Serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa yenye makao yake huko Tripoli mwezi Februari mwaka huu zilisaini hati ya maelewano kwa lengo la kutoa mafunzo, suhula na fedha za kuendeshea mapambano dhidi ya magendo ya binadamu. 
Hati hiyo ya maelewano imesainiwa kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya wakuu wa Umoja wa Ulaya huko Malta kwa shabaha ya kupambana na wahajiri kutoka Afrika kuelekea katika nchi za Ulaya. Viongozi wa Umoja wa Ulaya katika kikao chao huko Malta walikubaliana kupunguza wimbi la wahajiri wanaotoka nchini Libya.
Ili kutekeleza mpango huo, serikali ya Libya inatazamia kupokea yuro milioni 200 ili kutekeleza mpango huo, kukiwemo kukidhaminia fedha kikosi cha ulinzi cha pwani ya nchi hiyo. 
Wakati huo huo njia za baharini ambazo wahajiri walitumia kuelekea nchini Ugiriki mwaka uliopita wa 2016, hivi sasa zimefungwa baada ya kufikiwa makubaliano  kati ya viongozi wa Umoja wa Ulaya na Uturuki.
 Njia hizo zilikuwa njia muhimu zaidi ambazo wahajiri wamezitumia kuelekea katika nchi za Ulaya. 
Moja ya njia kuu zinazotumiwa na wahajiri kuelekea Ulaya ni ile ya kusafiri kwa boti kuanzia nchini Libya hadi Italia; njia ambayo hurahisisha biashara kwa magenge ya magendo ya binadamu. 
Umoja wa Ulaya unafanya kila uwezalo kutekeleza na nchi moja ya kaskazini mwa Kiafrika aina hiyo ya makubaliano iliyofikia na Uturuki kwa kuzingatia kuwa,  wahajiri wa Kiafrika wanaoelekea Ulaya wanatoka  katika baadhi ya nchi za Kiafrika zilizoathiriwa na machafuko ikiwemo Libya. 
Italia ambayo imesaini makubaliano na serikali ya Libya iliyo na makao makuu yake huko Tripoli  katika fremu ya siasa za Umoja wa Ulaya, ni moja ya nchi kuu za Ulaya ambazo wahajiri wa Kiafrika huzikimbilia. 
Hii ni katika hali ambayo serikali hiyo inayodhibiti eneo kubwa la ardhi huko Libya haina uwezo wa kudhibiti wimbi la wahajiri wala kuheshimu sheria za kibinadamu. 
Wakati huo huo Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) imetangaza katika taarifa yake kuwa Libya si mahali salama na kwamba kuwafungia njia watu wa nchi hiyo au kuwarejesha nchini humo ni sawa na kudhihaki thamani kuu za kibinadamu na utawala wa sheria. 
Serikali za Ulaya zimetoa taarifa na kuzungumzia kuboresha hali ya kambi za wakimbizi na kufuatilia hali ya kijamii na kiuchumi ya watu maskini katika nchi za kiafrika ili kudhibiti wimbi la wakimbizi wanaoelekea Ulaya katika hali amabyo maneno hayo yote yametolewa kipropaganda tu ili kuwanyamazisha watetezi wa haki za binadamu. 

chanzo:parstoday.

Comments