Korea Kaskazini imesema kuwa itajitetea kwa kutumia silaha kali ili
kujibu hatua ya Marekani kupeleka wanamaji wake katika rasi ya Korea.
Wizara ya maswala ya kigeni ilinukuu shirika la habari la serikali
KCNA lililosema kuwa hatua hiyo ya Marekani inaonyesha uvamizi wa
kijinga uliofika awamu yenye hatari kubwa.
Jeshi la Marekani katika maeneo ya Pacific limesema kuwa hatua hiyo inalenga kuonyesha Marekani imejiandaa kwa lolote lile.
Rais Trump amesema kuwa Marekani imejiandaa kibinafsi kukabiliana na tishio la nyuklia linaloletwa na Korea Kaskazini.
Wakati
huohuo Korea Kusini na China ambaye ni mwandani wa Korea Kaskazini
wameonya kuchukua hatua kali dhidi ya Pyongyang iwapo itafanya majaribio
zaidi ya makombora yake.
Kundi hilo la mashambulizi la Marekani kwa jina Carl Vinson Strike Group linashirikisha meli ya kubeba ndege za kivita.
Lilitarajiwa kuelekea nchini Australia lakini badala yake
likapelekwa magharibi mwa bahari ya Pacific ambapo hivi karibuni
lilifanya mazoezi ya kijeshi na wanamaji wa Korea Kusini.
''Tutailaumu
Marekani kwa matokeo mabaya yaliosababishwa na hatua yake'', ilisema
taarifa hiyo ya wizara ya maswala ya kigeni ilionukuliwa na shirika hilo
la habari la serikali KNCA.
chanzo:Bbc.
Comments