Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo hilo Mkuu wa Wilaya ya
Ilala, Sophia Mjema alisema, tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa
nane mchana huku chanzo kikiwa ni kuporomoka kwa udongo katika eneo
hilo.
Alisema baada ya tukio hilo kutokea waliwasiliana na Polisi kwa ajili
ya kufanya uokoaji ambapo walifanikiwa kuwatoa watu wawili ambapo mmoja
alitoka akiwa amevunjika na kukimbizwa katika Hospitali ya Amana na
mwingine akiwa amekufa na mwili wake kuhifadhiwa katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili.
“Kwa kweli ni tukio la kusikitisha lakini tunaendelea na jitihada za
kuwaokoa waliobaki ndani ya kifusi, Aprili 6 tulisitiza shughuli ya
uokoaji baada ya kuona udongo ukiwa unaendelea kuporomoka kila baada ya
dakika ishirini tukaona tusitishe kwasababu haikuwa salama, sasa hivi
tunasubiri tupate ‘escaveter’ na wataalamu ambao wataona ni jinsi gani
wataweza kuwaokoa wale waliobaki,”alisema Mjema.
Aliongeza kuwa eneo hilo sio rasmi kwa ajili ya uchimbaji wa kokoto
kwa kuwa tayari serikali ililifungia miaka miwili iliyopita lakini watu
hao waliendelea kufanya shughuli zao kwa kujiiba.
“Tumeshindwa kuelewa ni kwa nini watu hawa waliendelea kufanya
shughuli zao wakati tayari tulifunga eneo hili, tumepata taarifa kuwa
kuna mtu anadai eneo hili ni mali yake na alikuwa akiwaruhusu watu
kuingia kisha anawatoza fedha kwahiyo tutamtafuta na wale wote waliokuwa
wakirusu eneo hili kuendelea kufanya kazi tutawatafuta na hatua za
kisheria zitachukuliwa dhidi yao,”aliongeza Mjema.
Mjema alisema sio mara ya kwanza kutokea kwa ajali kama hiyo kwani
miaka miwili iliyopita ilitokea na kusababisha vifo vya watu kadhaa na
Mkuu wa Mkoa wa wakati huo, Said Meck Sadick aliamua kufunga machimbo
hayo.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji
Wilaya ya Ilala, Ully Mbuluko alisema, wanaendelea na jitihada za
uokoaji ambapo wanasubiri gari maalumu la uokoaji ili kuona namna ya
kuwafikia waliopo ndani.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi na kuwataka kuacha kuendelea na
shughuli katika eneo hilo kwakuwa tayari serikali walishalifunga miaka
miwili iliyopita ili kujiepusha na madhara yanayoweza kutokea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Salum Hamduni alikiri
kutokea kwa tukio hilo na aliwataja waliokuwa wamefukiwa kuwa ni Rashid
Fadhil (28), Amos Debwa (27)ambaye ametolewa akiwa amekufa, Boniface
Pius (30) na Shabani Omary (27) ambaye amevunjika mguu.
Alisema wanaendelea kushirikiana na idara mbalimbali za Serikali
ikiwemo Manispaa ya Ilala kuhakikisha miili hiyo inaokolewa na inakwenda
kuzikwa.
Hamduni alisema ili kudhibiti madhara mengine yasitokee jeshi hilo
litaweka ulinzi katika eneo hilo na yeyote atakaeingia katika eneo hilo
hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Gazeti hili lilipata fursa ya kuzungumza na baadhi mashuhuda wa tukio
hilo, Mohamed Seleman ambaye ni mmoja wa vijana wanaofanya shughuli zao
katika machimbo hayo alisema siku ya tukio hilo alitaka kufanya kazi
lakini moyo wake ulisita akaamua kuondoka lakini baada ya muda alirejea
na kushuhudia wenzake wakifukiwa.
“Tulikwenda kunywa chai pamoja lakini siku hiyo moyo wangu ulisita
kufanya kazi nikaamua kuondoka lakini wakati narudi ndio tukio likaanza
kutokea tuliamua kuwaokoa wenzetu na kufanikiwa kumtoa mmoja akiwa
amevunjika mguu wakati akijaribu kuruka,”alisema.
Alisema baada ya jitihada zao kushindwa waliamua kupiga simu Serikali
za Mitaa na walifika lakini waliona vifaa vinavyotumika kuokoa
havitaweza kufanya kazi hiyo hivyo walilazimika kuomba nguvu zaidi
kutoka Manipsaa ya Ilala na kufanikiwa.
Aidha, wananchi waliokuwepo kushuhudia tukio hilo walikiri kuzuiwa
kuendelea na shughuli katika eneo hilo lakini hali mbaya ya maisha
iliwafanya kuendelea.
Walisema kama serikali iliamua kuzuia machimbo hayo ilipaswa kurudi mara kwa mara ili kuangalia kama shughuli zinaendelea au la.
Gazeti hili pia lilifanya jitihada ya kufika katika Hospitali ya
Amana ili kumuona Omary ambaye Mkuu wa Wilaya alidai alipelekwa katika
Hospitali hiyo.
Ofisa Muuguzi wa zamu Getrude Massawe alikiri kumpokea Omary majira
ya saa kumi jioni akiwa amevunjika mguu wa kulia lakini alihudumiwa na
kuruhusiwa kuondoka kwa kuwa hakuwa katika hali mbaya.
chanzo:Habarileo.
Comments