Kabudi aanza na Katiba mpya.

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi (wa pili kushoto) akiwasilisha kwa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria taarifa ya mpango na makadirio ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2017/18 mjini Dodoma. Kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Amon Mpanju, Naibu Mwanasheria wa Serikali, Gerson Mdemu na Mkurugenzi wa mashtaka wa Serikali (DPP) Biswalo Mganga. (Picha na Mroki Mroki).SERIKALI inapitia sheria zinazohusika na mchakato wa mabadiliko ya Katiba kubaini utaratibu mzuri wa kuendelea na mchakato huo kwa hatua ya kupiga kura ya maoni kwa Katiba Inayopendekezwa.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa, kuchelewa kwa hatua hiyo kumetokana na dhamira njema ya Serikali ya Awamu ya Tano kutaka kuboresha mifumo na miundo ya kiutendaji nchini.


Akihutubia Bunge baada ya kuapishwa Novemba 5, 2015, Rais John Magufuli alisema Serikali yake inatambua mchakato wa kupata Katiba mpya na itaendelea nao.

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, ameiambia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano inatambua umuhimu wa nchi kuwa Katiba mpya.

“Hata hivyo ikumbukwe kuwa mara baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani, ilianza kazi kwa kuunda serikali, uhakiki wa watumishi hewa, uadilifu na kupunguza Baraza la Mawaziri ili kuongeza uwajibikaji,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema ingawa lengo la serikali halikuwa kupunguza idadi tu ya watendaji na viongozi, lakini kupunguza idadi ya mawaziri kutoka 60 hadi 18 ni moja ya dhamira ya mageuzi katika utendaji na uwajibikaji.

Alisema hivi sasa, baada ya kazi hiyo kukamilika, Serikali inapitia sheria zote zinazohusika na mchakato huo wa mabadiliko ya Katiba kubaini utaratibu mzuri wa kuendelea na mchakato huo kutoka pale ulipoishia,” alisema.

Profesa Kabudi alieleza hayo wakati akijibu hoja za wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge ya Sheria na Katiba kuhusu mchakato huo baada ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2016/17 na mapendekezo kwa mwaka 2017/18 mbele ya kamati hiyo mjini hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasilisha taarifa hiyo, Profesa Kabudi alisema: “Serikali inalipa uzito mkubwa suala la Katiba mpya, ila serikali ilikuwa na kazi ya kuunda mifumo na baadhi ya mageuzi ya kimfumo yamegusa matakwa ya Bunge Maalum la Katiba kuhusu Katiba mpya ambalo nami nilikuwa mjumbe.

“Hivi sasa kutokana na mabadiliko ya sheria mbalimbali, maboresho ya uadilifu serikalini ambao wajumbe wa Bunge la Katiba mpya walilipigia kelele sana tayari limetekelezwa na aina namna ya utendaji makosa sasa imebadilika si kama miaka 20 iliyopita.

“Aina ya uchumi nayo imebadilika kutoka katika mfumo wa ujamaa na chama kimoja hadi wakati tulio nao sasa, matamanio ya rushwa yameongezeka na kazi ya kuyadhibiti inaonekana, wakati haya yakiendelea kufanywa na Serikali, suala zima la kupitia na kushauri Serikali namna njema ya kuendelea na mchakato, linaendelea,” alisema Profesa kabudi.

Alifafanua kuwa, lengo kubwa la Katiba ni kuleta mabadiliko katika sekta zote nchini, na baadhi yameanza kuonekana ikiwemo maadili ya viongozi wa umma yamerejea na sasa viongozi wanatamka viapo na kuvisaini.

Wakati wa wajumbe wa kamati wakijadili, Mbunge wa Bahi, Omary Badwel (CCM) alishangaa kwa nini wizara haijatenga muda maalum wa kukamilisha kupatikana kwa Katiba mpya wakati ipo wazi katika Ilani ya CCM ya 2015-2020.

“Jamii ina matarajio makubwa ya kupatikana kwa Katiba mpya kabla ya awamu hii ya uongozi kwa kuwa Ilani ya CCM imeahidi hayo lakini Serikali imekaa kimya kuhusu muda, haijaainishwa wazi lini tutapata hiyo Katiba mpya katika mpango wa wizara. “Tunahitaji kuona mchakato wa kupata Katiba mpya unakamilika ndani ya awamu hii,” alisema Badwel.

Akijibu hoja hiyo ya Badwel, Profesa Kabudi alisema kama alivyofafanua katika taarifa, mchakato utaendelea lakini yeye kwa kuwa ni mgeni kwenye wizara, hawezi kueleza ni lini.

“Nadhani kwa kuwa mimi ni mgeni katika wizara, nitayachukua haya maana hata Waziri Mkuu zijamuona, vikao vya Baraza la Mawaziri sijakaa. Makamu wa Rais nimeonana naye siku ya kuapishwa. Naomba niahidi kulifanyia kazi zaidi hili,” alisema Profesa Kabudi.

Katiba mpya itakapokamilika, itaiondoa Katiba ya mwaka 1977 inayotumika hivi sasa ambayo wakati ikitungwa, mfumo wa uongozi nchini ulikuwa ni wa chama kimoja.

Hata hivyo Katiba hiyo imefanyiwa marekebisho kadhaa kukidhi kwa sehemu kubwa mahitaji ya wakati huu.

Miongoni mwa wadau wanaosimamia kupata Katiba mpya ni Jukwaa la Katiba Mpya, ambalo limeendelea kuishauri Serikali kutenga fedha maalum katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/18 kwa ajili ya kuendelea na mchakato wa kupata Katiba mpya, hatua ya kura za maoni kwa Watanzania.

Waziri Kabudi aliwasilisha taarifa kwa kamati inayoonesha kuwa wizara hiyo inahitaji bajeti ya Sh bilioni 159.31 ikiwa na upungufu wa asilimia 4 ya bajeti ya mwaka jana ya Sh bilioni 191.4.
chanzo:Habarileo.

Comments