Hili ni Jukwaa la pili la Biashara lililoandaliwa na Kampuni ya
Magazeti ya Serikali (TSN) kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza. Jukwaa la kwanza kuandaliwa na TSN lilifanyika Februari 13
mkoani Simiyu na kuhudhuriwa na watu takribani watu 160.
Makundi mbalimbali kuhudhuria Maandalizi kamambe yanayoendelea hapa
mkoani Mwanza yanaonesha kwamba washiriki wanaotazamiwa kuketi kwa saa
kadhaa wakifaidikia na uwepo wa Jukwaa hilo la Biashara ni pamoja na
wafanyabiashara wadogo wakiwemo madereva wa bodaboda, teksi na daladala.
Pia kutakuwa na wauza bidhaa kwenye masoko mbalimbali mkoani Mwanza,
wauza mitumba na wauza samaki na dagaa. Kwa mujibu wa Mhandisi Boniface
Nyambele anayeratibu Jukwaa hilo kwa upande wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na
Patrice Simbachawane wa TSN, wengine walioalikwa ni wafanyabiashara
wakubwa na wa kati, wafanyabiashara wanawake na wamiliki wa viwanda.
Mkoa wa Mwanza una viwanda 86 kwa mujibu wa Kitengo cha Uwekezaji
mkoani Mwanza kinachoongozwa na Mhandisi Nyambele sambamba na maofisa
wengine waandamizi sita.
Waratibu hao tayari wamesambaza pia barua za mwaliko kwa wawakilishi
wa taasisi mbalimbali za elimu mkoani Mwanza, maofisa mbalimbali wa
taasisi za serikali, maofisa wa halmashauri nane za mkoa wa Mwanza,
wakuu wa wilaya, wabunge na wakuu wa mikoa ya jirani.
Wengi watajaribu uwekezaji mkubwa Akizungumzia matarajio yake kuhusua
Jukwaa hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella anasema ana
matumaini makubwa kwamba litawazindua wafanyabiashara wazawa kufikiria
kufanya makubwa zaidi kwa faida yao, mkoa na taifa kwa ujumla.
Anasema anatamani kuona wafanyabiashara wadogo wanatumia fursa
zilizopo kwa kuwekeza pakubwa na hivyo kuwa pia wafanyabiashara wakubwa.
Mkuu huyo wa mkoa anasema pamoja na kukaribisha wawakezaji wengine
kutoka nje ya mkoa na hata nje ya nchi, angetamani kuona wawekezaji wa
mkoani mwake wanakuwa wa kwanza kunufaika na fursa zilizopo.
“Kimsingi, tunao wawekezaji wengi wazalendo na wazawa wa hapa Mwanza.
Na hata pesa wanazo lakini bado wanahangaika na vitu ambavyo havina
tija kubwa kwao wenyewe, kwa mkoa na taifa kwa ujumla.
Tunataka jukwaa hili lisaidie kuwabadilisha, wazione fursa na kuwa
wawekezaji wakubwa. “Kwa lugha nyingine, wawekezaji wa ndani (hapa
mkoani Mwanza) wapo lakini tatizo lao ni namna gani waingie kwenye
uwekezaji mkubwa. Nina imani kwamba jukwaa litasaidia kuwabadilisha hawa
wawekezaji wetu wa ndani,” anasema.
Mkuu huyo wa mkoa anawakaribisha wote waliopata mwaliko na
watakaoendelea kupata wahakikishe hawakosi kuhudhuria jukwaa hilo adhimu
kwa ajili ya maendeleo yao na ya mkoa kwa ujumla. Baadhi ya wadau
watakaotoa elimu muhimu kwa wafanyabiashara ni pamoja na benki za NMB,
TIB (Development), TIB (Corporate) na Benki ya TPB.
Taasisi hizi za fedha zinatazamiwa kueleza, pamoja na mambo mengine,
namna wafanyabiashara wanavyoweza kupata fedha za mitaji alimradi waweze
kutekeleza masharti fulani fulani.
Ni uelewa kwa kwenda mbele Katika Jukwaa la Simiyu, Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya TIB (Corporate), Frank Nyabundege alisema kwamba
mtu akitekeleza masharti ya benki hiyo ambayo pia inatoa huduma ya
kuandaa maandiko ya miradi kitaalamu, anaweza kupata mkopo ndani ya siku
mbili.
Nyabundege akaweka wazi kwamba benki yao ndio ipo mahususi kwa ajili
ya suala zima la kutekeleza dhana ya viwanda inayotekelezwa na serikali
ya awamu ya tano.
Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha wateja wakubwa wa NMB, Nsolo Mlozi,
atakuwepo Mwanza kuongeza uelewa kwa Watanzania hao zaidi ya 300 kuhusu
masuala mbalimbali ya kibenki na namna wanavyoweza kupata mitaji kupitia
NMB.
Hivi karibuni alipozungumza na HabariLeo, Mlozi alisema: “Cha muhimu
ni uelewa kwa wananchi...
Tunakwenda pia kulifanya hilo (la kuamsha
uelewa) Mwanza.” Mamlaka ya Mapato (TRA) ni mdau mwingine wa maendeleo
anayetazamiwa kutoa elimu muhimu kwa mlipa kodi.
Kama ilivyotokea Simiyu, ni taasisi inayotazamiwa kuulizwa maswali
mengi na wafanyabiashara Taasi hiyo inaamini kwamba wananchi wengi wanao
utayari wa kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yao alimradi tu
wajue taratibu muhimu na kanuni.
Wakati Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) linatazamiwa
kueleza mengi namna wana- Mwanza wanavyoweza kulitumia katika
kufanikiwa, Bohari ya Dawa (MSD) itaeleza, pamoja na mambo mengine,
namna ambavyo watu binafsi wanaweza kununua vifaa tiba kutoka kwenye
bohari hilo badala ya kuhangaika kwenye maduka binafsi.
Bila afya, huwa ngumu kuendesha biashara kwa ufanisi hivyo Mfuko wa
Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), utatumia jukwaa hilo kueleza namna
wafanyabiashara na makundi mbalimbali ya wajasiriamali wanavyoweza
kufaidika nao, wakapata matibabu hata wakati ambao hawana fedha mfukoni.
Katika muktadha huo wa afya, taasisi ya Ariel Glaser Pediatric Aids
Healthcare Initiative (AGPAHI), pamoja na mambo mengine, itawajuza
washiriki kwamba ili nguvu kazi iwe na manufaa ni lazima iwe na afya
njema.
Miongoni mwa mengi yatakayosemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dk
Sekela Mwakyusa ni: “Tumekuwa huku Kanda ya Ziwa kwa muda sasa,
tumejionea mengi mintarafu suala zima la Ukimwi lilivyo. Wengi hawajui
hali ilivyo.”
Watumishi Housing Company (WHC) itaeleza namna inavyojenga nyumba za
kisasa katika eneo la Kisesa mkoani Mwanza na jinsi inavyopania
kuwawezesha watu binafsi kununua hisa (vipande) katika kuchangia makazi
bora.
Nao Mfuko wa Pensheni wa LAPF utawataka wawekezaji wachangamkie
kukodi maduka katika ukumbi wa Rockcity Shopping and More kwani bado
yapo yaliyo wazi ili kupata mafanikio makubwa kibiashara. Pia wataeleza
mafao wanayotoa kwa wafanyakazi wanaojiunga na mfuko huo.
Baraza la Biashara Tanzania litakuwa na mengi ya kuzungumza na
wafanyabiashara wenzao huku Kampuni ya Simu (TTCL) ikielezea jinsi
wafanyabiashara wanavyoweza kufaidika nayo kupitia bidhaa nyingi
inazotoa kwa sasa.
Je, ni wangapi wanajua kwamba TTCL imeanzisha huduma ya kutuma pesa
na ambayo ina faida maradufu kwa mteja? Je, unajua kwamba ukitaka
kujiunga na mkonga wa taifa ni suala la kuwasiliana nao tu bila
kuuhangaika kwingineko?.
Kampuni ya simu ya Vodacom, moja ya mitandao pendwa nchini pia
itaeleza namna inavyorahisisha maisha hususani kwa wafanyabiashara huku
Mfuko wa Pensheni wa PPF ukieleza mafao mengi ambayo watanzania
wanaojiunga nao wanafaidika. Mengi zaidi kuhusu Jukwaa la Biashara
Mwanza endelea kusoma HabariLeo.
chanzo:Habarileo.
Comments