Jando na unyago kupigwa marufuku wakati wa masomo.

SERIKALI wilayani Tunduru katika Mkoa wa Ruvuma imepiga marufuku shughuli zote za jando na unyago kufanyika wakati wa masomo na kuagiza kuanzia sasa shughuli hizo zifanyike wakati wa likizo ili kutoa fursa kwa wanafunzi kuhudhuria masomo yao darasani.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Homera amesema kutokana na wilaya hiyo kuendelea kufanya vibaya kitaaluma na kuwa miongoni mwa wilaya zilizofanya vibaya katika mitihani mbalimbali ya mkoa na taifa kutokana na shuhuli hizo kufanyika zaidi wakati wa masomo jambo ambalo linawakosesha masomo wanafunzi hao.


Akizungumza kwa njia ya simu, Homera alisema ni muda mrefu Wilaya ya Tunduru iko nyuma kielimu ikilinganishwa na wilaya nyingine za Mkoa wa Ruvuma huku chanzo kikitajwa ni mwamko mdogo wa elimu kwa wazazi, walezi na jamii mzima ya watu wa wilaya hiyo.

Alisema kwa sasa timu ya viongozi ya Awamu ya Tano ikiongozwa na yeye mwenyewe pamoja na wataalamu wengine wa halmashauri imeweka mikakati kabambe kama vile kuhakikisha shule zote za msingi na sekondari zinatoa chakula cha mchana kwa wanafunzi baada ya kubaini kwamba chanzo cha kufanya vibaya na utoro kwa baadhi ya watoto ni kutopata chakula cha mchana.

Alisema hakuna sababu ya msingi kwa Wilaya ya Tunduru kuendelea kufanya vibaya kitaaluma kwa kwani ni kati ya wilaya zenye fursa nyingi ambazo kama zikitumika vizuri zitasaidia kuharakisha kukua kwa uchumi kuanzia ngazi ya familia, wilaya na mkoa..

Aidha, alisema kukamilika kwa mtandao wa uhakika wa barabara ya lami kutoka Tunduru hadi makao makuu ya mkoa mjini Songea na barabara kutoka Tunduru hadi Dar es Salaam kupitia mikoa jirani ya Lindi na Mtwara ni fursa mojawapo ambayo inaweza kuharakisha maendeleo.
chanzo: zanzibar24.

Comments