
Alisema wakati Wajumbe wa Tume hiyo wakijipanga kuingia kwenye vita hivyo waelewe kwamba wanaingia katika vita vikali vya kupambana na wenye fedha nyingi na mtandao wa siku nyingi.
Akiizindua rasmi Tume hiyo ya Kitaifa ya kuratibu na kudhibiti dawa za kulevya hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar akiwa yeye ndie Mwenyekiti wa Tume hiyo Balozi Seif Ali Iddi alisema mafanikio ya Tume hiyo yatategemea zaidi jinsi wajumbe wake watakavyojipanga vizuri kwa kushirikiana kwa karibu zaidi na wadau wengine katika kukabiliana na uingizwaji wa dawa hizo Nchini.
Balozi Seif alisema hali ya utumiaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini kote sio mzuri hali iliyopelekea Serikali zote mbili kulivalia njuga tatizo hilo sugu la Dawa za kulevya lenye kuiangamiza jamii hasa Vijana ambao ndio nguvu kazi kubwa ya Taifa.
Alisema kwa kuwa wanaojishughulisha na dawa za kulevya baadhi yao wanaeleweka na wanaishi pamoja na jamii Mitaani. Hivyo ni vyema jukumu la Wajumbe wa Tume hiyo likaelekeza zaidi nguvu zake katika uzuiaji wa uingizaji wa dawa hizo hapa nchini sambamba na kutoogopa kuwachukulia hatua za kisheria wahusika hao.
Balozi Seif alisisitiza kwamba kwa kuwa suala la dawa za kulevya linazikumba pembe zote za Dunia, mafanikio ya vita hivyo yatahitaji mashirikiano ya Taasisi za ndani na nje ya nchi ambazo zinajihusisha moja kwa moja na dawa hizo thakili.

Aidha Balozi Seif aliwapongeza Wajumbe wote walioteuliwa kushirikiana naye katika utekelezaji wa jukumu hilo zito ambalo anaimani kwamba kila mjumbe analiweza licha ya uzito uliopo mbele yao.
Balozi Seif aliwakumbusha Wajumbe wa Tume hiyo wajibu wao kwa Mujibu wa Kifungu cha 4 {1} cha Sheria wa kusimamia mambo Tisa akiyataja baadhi yake kuwa ni pamoja na kuandaa na kusimamia utekelezaji wa mpango wa Taifa za Udhibiti wa Dawa za kulevya.
Nyengine alisema ni kupitia sheria na kanuni za Udhibiti wa dawa za kulevya, kuimarisha na kuendeleza jitihada za kuzuia matumizi ya dawa za kulevya, kuanzisha mfumo wa ukusanyaji na uchambuzi wa Taarifa za matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya.

chanzo:zanzibar24.
Comments