
Dk. Shein aliyasema hayo katika hafla ya uzinduzi
wa barabara ya Mgagadu-Kiwani, Mkoa wa Kusini Pemba, iliyojengwa kwa
fedha za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambapo kazi za ujenzi imefanywa
ka kusimamiwa na Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji kupitia
Idara ya Ujenzi an Utunzani UUB.
Katika hotuba yake kwa wananchi, Dk. Shein aliwaeleza wananchi kuwa
wakati wa kupiga siasa umekwisha na kilichokuwepo hivi sasa ni kufanya
kazi kwa kila mmoja alieajiriwa na asieajiriwa na wale
wanaojishughulisha na kilimo waendelee na shughuli zao hizo kwa lengo la
kujiletea maendeleo.
Alisema kuwa uchaguzi haupo tena hadi mwaka 2020 na kuongeza kuwa
vyama vya siasa vipo lakini hakuna chama kitakacholeta Serikali nyengine
kwani tayari Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo madarakani ambayo
imekuwa ikiwaheshimu na kuwapelekea maendeleo wananchi popote pale
walipo.
Dk. Shein alisema kuwa yeye ndie Rais wa Zanzibar na kila analosema
ana uhakika nalo kwani hana kawaida ya kusema uwongo, hivyo aliendelea
kuwaasa wananchi kisiwani humo kuendelea na shughuli zao na kutosikiliza
tumbaku za mitaani.
“Wananchi wafanye kazi na zingatieni maelezo ninayosema mbali ya kuwa
mimi ndie Rais wenu pia, ni mwenenu na ndugu yenu…mjue kuwa hapa hakuna
Serikali nyengine itakayokuja kwani serikali halali ya Mapinduzi ya
Zanzibar ipo na itaendelea kuwepo”alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein aliwaeleza wananchi katika hafla hiyo kuwa barabara
hiyo ni ya watu wote na waitumie kwa maslahi yao kwani fedha
zilizojengewa zinatokana na kodi za wananchi wa Unguja na Pemba huku
akiwataka waitunze na kuienzi.
Alisema kuwa Serikali inaendelea kutimiza ahadi yake ya kuwapelekea
wananchi maendeleo huku akiwaeleza wananchi kuwa bado ujenzi wa barabara
nyengine muhimu unaendelea tena kwa kiwango cha lami kisiwani humo.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwaeleza wananchi wa Kiwani na vitongoji
vyote ilikopita barabara hiyo, kuanzia Mgagadu, Kivumoni, Minazini,
Kirimdomo, Kendwa, Jundamiti hadi kufikia Kiwani Pwani kuwa kufunguliwa
kwa barabara hiyo ni furaha kubwa kwao.
Miongoni mwa barabara ambazo Dk. Shein alizitaja kuwa zimo katika
ujenzi ni barabara ya Ole-Vitongoji, Pujini hadi Kengeja yenye kilomita
35 imeanza kwa kifusi na baadae itatiwa lami huku akieleza azma ya
ujenzi wa barabara ya Chake Chake-Ziwani hadi Wete nayo itajengwa kwa
kiwango cha lami ambapo ujenzi wake utaanza si muda mrefu.
Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar inaendelea kwa kasi kubwa katika
kuimarisha sekta zake za maendeleo na kuwahakikishia wananchi kuwa ahadi
zote zilizoahidiwa zitatekelezwa.
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwaahidi wananchi wa Kiwani kuwa kisima
chao kitatiwa umeme chini ya miezi miwili na nyumba ya daktari
itajengwa, ahadi hizo zinatokana na ombi la wananchi hao lililotolewa na
Mzee Omar Khamis ambaye nae alitumia fursa hiyo kumshukuru Dk. Shein
kwa niaba ya wananchi wa Kiwani.
Nae Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Balozi Ali Karume
alisifu mashirikiano makubwa yaliopo katika Wizara yake hali ambayo ndio
chachu ya mafanikio katika Wizara hiyo.
Balozi Karume alisifu juhudi za Dk. Shein za kutekeleza ahadi
anazoziahidi na kueleza kuwa ni kiongozi wa pekee anaefuatilia kwa
karibu miradi ya maendeleo katika Serikali anayoiongoza huku akisisitiza
umuhimu wa uzalendo.
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji
Mustafa Aboud Jumbe akitoa taarifa fupi juu ya ujenzi wa barabara hiyo
alisema kuwa ujenzi huo ni mojawapo ya jitihada ambazo Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikichukua tokea Mapinduzi ya Zanzibar ya
mwaka 1964 ya kujenga ustawi wa wananchi katika kuimarisha miundombinu
ya barabara za mijini na vijijiji kwa Unguja na Pemba.
Alisema kuwa ujenzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya
maendeleo, Mkuza III, Sera ya Taifa ya Usafiri pamoja na Mpango Mkuu wa
Usafiri Zanzibar na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi.
Aliongeza kuwa Mradi wa ujenzi wa barabara ya Mgagadu-Kiwani ulianza
rasmi mwaka 2009 na umechukua muda mrefu kukamilika kutokana na
changamoto mbali mbali zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wake.
Katibu huyo alieleza kuwa Februari 2017 barabara hiyo imekamilika
rasmi kwa kiwango cha lami mpaka pwani ambapo ujenzi wake ulikuwa wa
awamu tatu.
Mradi huo umefadhiliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia
fedha za maendeleo kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina kwa hatua ya awali pamoja
na Mfuko wa Barabara Zanzibar kwa hatua za ukumilishaji wa ujenzi kwa
gharama za Tsh Bilioni 1.4 .
Alieleza kuwa Barabara hiyo ina kilomita 8.85 ambapo hapo awali
ilipangwa kujengwa kilomita 7.6 na ongezeko la kilomita 1.25 limekuja
kutokana na agizo la Rais mara baada ya wananchi wa Kiwani Likoni
kumuomba barabara hiyo iwekwe lami hadi pwani na yeye alikuba kutokanan
na umhimu wake.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
chanzo: zanzibar24.
Comments