Dk Bilal ataka ajira zizalishwe zaidi.

Makamu wa Rais mstaafu, Dk Mohammed Gharib BilalSERIKALI na taasisi binafsi zimeombwa kuzalisha ajira kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalumu ikiwemo wenye usonji, waliopatiwa mafunzo katika shule mbalimbali nchini ili kuwawezesha kuishi maisha kama watu wengine.

Hata hivyo, serikali imesema kuwa itaendelea kuipa kipaumbele elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu na kuunga mkono shule za Al-Muntazir kama mfano kwa kusaidia kutoa elimu na mafunzo kwa watoto hao.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam na Makamu wa Rais mstaafu, Dk Mohammed Gharib Bilal, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Usonji Duniani yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Khoja Shia Itha Asheri Jamaat (KSIJ) na kufanyika katika Shule ya Al Muntazir ikiwa na kaulimbiu ya “Tuwalinde na Tuwapende.”
Dk Bilal alisema shule hiyo imekuwa kwa kasi na wanaelekea kwenye uzalishaji wa miradi mbalimbali ikiwemo viwanda vidogo vidogo ambapo watoto wenye mahitaji maalumu watapata fursa ya kujipatia ajira itakayowaingizia kipato kama watu wengine.
Alisema kwa kufanya hivyo itawapatia wazazi wenye watoto wa aina hiyo chachu ya kuwatoa nje kwa madhumuni ya kuwapatia elimu kwa ustawi wa maisha yao.
“Nitapeleka maombi yenu na nitafuatilia serikalini waweze kuwasaidia kupata maelezo ya shule zote zinazotoa huduma ya aina hii ili kujenga mahusiano na kuipa Shule ya Al-Muntazir jukumu la kuwa kiongozi wa mtandao huu,” alisema Dk Bilal.
Pia alisema wadau mbalimbali wanapaswa kuunga mkono jitihada za shule hizo kwa kuwa inahitaji gharama kubwa katika kuendesha shule hizo.
Alifafanua kuwa shule hiyo imekuwa ikijumuisha watoto wenye mahitaji maalumu kwenye madarasa ya kawaida ili wapate mafunzo ya pamoja na kuwapatia fursa ya kujifunza na watoto wengine.
‘’Watoto hawa ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwani wazazi wanaopewa watoto hawa wanaangaliwa namna watakavyowalea na kuwahudumia. Wanapaswa kutunzwa kwa upendo, amani na kuwatoa nje ili wajumuike na wengine kwa kuwapatia elimu kwa kiwango kinachotakiwa,’’ alieleza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya KSIJ na shule za Al Muntazir, Imtiaz Lalji alisema katika shule yao inayotoa mafunzo maalum kwa watu wenye ulemavu ya Amsen imefanikiwa kufundisha watoto 80 kwa kutumia vifaa maalum pamoja na walimu waliobobea.
Lalji alisema lengo lao ni kuhakikisha wanakidhi matarajio ya watoto hao ili kukithi mahitaji yao ya ajira kwa kupata elimu bila kikwazo.
“Katika shule zetu za Al Muntazir kuna wanafunzi zaidi ya 4,500 ambapo tumetoa ajira zaidi ya 500 kwa walimu na wafanyakazi wengine kwa ajili ya kupigani ubora wa shule zetu. Tunapokea watoto wenye mahitaji maalumu kuanzia miaka mitatu hadi 22 kwa ada ya shilingi milioni tatu pekee ambapo tunaendesha kwa hasara ya shilingi milioni 3.5,” alifafanua Lalji.
Aliomba serikali kuwasaidia kupatiwa ruzuklu kutoka mashirika mbalimbali ili kuendeleza jitihada zao za kuboresha elimu kwa watoto hao.
Alisema njia bora ya kuwalinda watu tuwapendao sio kwa kuwaweka mbali na watu wengine bali ni kwa kuwatoa nje waonane na jamii, wakubalike na kuwa sehemu ya jamii.
“Watoto hao wanatutegemea kwa ajili ya usalama wa maisha yao na jinsi gani tunawasaidia kuwatayarisha kufika ndoto zao za baadaye. Kuwaacha ndani haitasaidia tunakosa upendo kwao,” aliongeza.
chanzo:Habarileo.

Comments