DC aja juu utunzaji wa mazingira.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo.MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo amemuagiza Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mngazi, Tarafa ya Bwakila katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Neema Marundo kusimamia sheria za mazingira na kuhakikisha miti inapandwa eneo la mita 60 za mto Mngazi ili kudhibiti uharibifu wa mazingira.

Chonjo alitoa agizo hilo juzi alipotembelea maeneo yaliyoathirika na mafuriko ya mvua ambayo yalisababisha kaya 17 kwenye vijiji vya kata hiyo kukosa makazi baada ya nyumba kubomolewa.


Mafuriko hayo ya mvua zilizotokea mwanzoni mwa Aprili mwaka huu yamesababisha pia akiba ya chakula kilichokuwa kimehifadhiwa katika nyumba hizo kuharibiwa na maji ikiwa na kuharibu ekari zaidi ya 20 za mazao mbalimbali.

Mkuu huyo wa wilaya alisema licha ya kutokea kwa mafuriko hayo na kuathiri baadhi ya kaya za wananchi katika kata hiyo, hali hiyo imechangiwa pia na uharibifu wa mazingira kando kando ya mto na meneo mengine ya milimani.

Kutokana na hali hiyo, alimwagiza Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo kusimamia sheria za mazingira kuhakikisha miti inapandwa eneo la mita 60 la mto na kabla ya kupanda miti hiyo alimtaka apate kwanza ushauri wa aina ya miti inayofaa na rafiki wa mazingira.

“Eneo hilo la mita sitini kutoka kwenye mto kila upande ipandwe miti na mpate kwanza ushauri wa wataalamu wa misitu wakiwemo wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ili kuona ni aina gani ya miti inayofaa kupandwa itakayokuwa ni rafiki wa mazingira,” alisema Chonjo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Sudi Mpili alisema athari za mafuriko hayo zimechangiwa na uharibifu wa mazingira hasa maeneo ya mito na ukataji wa miti misitu ya asili.
 chanzo:Habarileo.

Comments