Chanjo mpya dhidi ya maradhi ya mtoto kutolewa Zanzibar.

Shirika la Afya Duniani WHO kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Watoto UNICEF na wadau wengine mbalimbali wameanzisha chanjo mpya dhidi ya maradhi yanayoonekana kuathiri sana afya ya mtoto ulimwenguni.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman wakati alipokuwa akizindua wiki ya Chanjo ya Afrika huko Kituo cha Afya Kinuni Mtofaani Wilaya ya Magharibi “A” Unguja.


Amesema chanjo hizo mpya ni pamoja na chanjo ya Nimonia na kuharisha kwa watoto umri wa mwezi mmoja na nusu ambazo zinatolewa bure katika vituo vyote vya Afya mjini na vijijini ili kuweza kuwakinga na maradhi yanayojitikeza kila siku.

Alisema lengo la wiki ya chanjo Afrika ni kuongeza msisitizo juu ya umuhimu wa chanjo katika kuokoa maisha ya watoto na kupata chanjo zao kwa wakati uliopangwa.

Alisema kuwa Wizara ya Afya kupitia kitengo chake Chanjo imeweka mazingira mazuri kuhakikisha huduma za chanjo kwa watoto  zinapatikana kwa urahisi na uweledi mkubwa katika vituo vyote.

Alieleza chanjo hizo zinazotolewa katika zoezi hilo zinajumisha aina zote za chanjo za kawaida zinazotolewa kila siku katika vituo vya ikiwemo Polio, kifua kikuu, Pepopunda, Dondakoo, Kifaduro, Homa ya Ini, Homa ya Uti wa mgongo, Surua Rubella, Nimonia na Kuharisha.

“Wiki hii ina umuhimu mkubwa katika mustakbali wa maisha ya watoto wetu hapa Zanzibar, sote kwa ujumla tuna jukumu la kuwalinda watoto wetu dhidi ya maradhi mbalimbali kwa kuhakikisha wanapata chanjo zote zinazostahiki tena kwa wakati uliopangwa,” alisisitiza Bi Harusi.

Naibu huyo alisistiza watoto wote walio chini ya umri wa miaka miwili ambao hawakuweza kupata chanjo wapelekwe katika vituo vya afya kwa ajili ya kupata chanjo hizo ambayo ni haki ya msingi kwa kila mtoto kwani kukosa haki hiyo ni kumuhatarishia afya yake pamoja na maambukizi ya maradhi .

“Takwimu za chanjo za mwaka 2016 zinaonesha kuwa bado kuna wilaya na baadhi ya vituo vya afya havikufikia kiwango cha chanjo kilichotakiwa hivyo nitoe wito kwa wilaya hizo na pamoja na vituo vyote vya afya vitumie nafasi hii ya wiki ya chanjo Afrika kuhamasisha jamii na familia kuhusu umuhimu wa kupata chanjo hizo,”alieleza Naibu huyo wa Afya

Hata hivyo Naibu  Harusi alifahamisha kuwa Serikali inategemea kuanza kutoa huduma ya chanjo ya kujikinga na saratani ya shingo ya mlango wa kizazi  kwa kina mama wenye uwezo wa kuzaa ifikapo mwaka 2018 hivyo ni jukumu la kina mwananchi kuelimishana juu ya umuhimu wa chanjo.

Hata hivyo amliwataka viongozi na watendaji wa ngazi zote kutoa ushirikiano katika kuhakikisha kuwa wananchi wanahamasika katika kushiki chanjo hizo ili kufikia lengo lililokusudiwa la kutokomeza maradhi kwa watoto.

Akitoa maelezo mafupi kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Kinga bi Atie Juma Shaame alisema serikali inachukua juhudi kubwa katika kupiga vita na kuondoa maradhi  kwa kutoa  chanjo dhidi ya watoto hivyo wananchi wasipuuze  kuwapeleka katika vituo vya afya ili kuweza kupata Taifa bora lenye afya njema.

Alisema chanjo ni kitu muhimu kwa maisha ya binadamu katika kujikinga na maradhi mbalimbali ambayo itamwezesha kuishi katika afya nzuri na kuepukana na maambuzi yanayoweza kuepukika.

Nae Mwakilishi kutoka Shirika la Kuhudumia watoto Duniani UNICEF Shemsa Nassor Mselem amesema shirika lake litaendelea kutoa ushrikiano na serikali ili kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata chanjo ambayo ni haki yake ya msingi na hasa wale wanaoishi katika mazingira hatarishi wasikose kupata haki yao hiyo.

IMETOLEWA NA MAELEZO ZNZ.
chanzo: zanzibar24.

Comments