Spika wa Bunge, Job Ndugai aliliambia gazeti hili kuwa ataunda kamati hiyo teule mwezi Juni mwaka huu.
Awali alitangaza kuunda kwa kamati hiyo mara baada ya kutembelea
Bandari ya Dar es Salaam na kujionea kontena zaidi ya 250 za mchanga wa
dhahabu zilizokuwa zisafirishwe nje ya nchi zikiwa zimezuiwa bandarini
hapo.
“Kamati yetu itaangalia kwa mapana zaidi juu ya sheria za madini na
mikataba,” alisema Ndugai wakati akijibu ujumbe mfupi wa maneno
aliotumiwa na gazeti hili.
Gazeti hili lilikuwa linataka kufahamu iwapo azma ya Bunge ya kuunda
kamati bado ipo pale pale licha ya serikali kutangaza kuunda kamati
mbili.
Rais Magufuli ameshaunda tume ya kwanza inayohusisha wanasayansi wa
jiolojia, kemia na wachambuzi wa miamba ambao majukumu yao ni kuchunguza
kilichomo kwenye mchanga unaosafirishwa nje kwa ajili ya kwenda
kuchenjuliwa makinikia ya shaba.
Tume hiyo inayoongozwa na Ofisa Mtendaji wa Wakala wa Jiolojia (GST),
Profesa Abdulkarim Mruma na imepewa siku 20 kuhakikisha inawasilisha
ripoti yake kwa Rais.
Rais wakati anaiapisha tume hiyo alitaka asiwemo mtu yeyote wa
kuizuia kutekeleza wajibu wake na iende sehemu yoyote kuchukua sampuli
kwa kadri itakavyoona inafaa.
Rais pia alitangaza kuwa hivi karibuni ataunda tume ya wataalamu wa
masuala ya uchumi ambao watachunguza mikataba na namna Tanzania
inavyofaidika na usafirishaji huo wa mchanga nje ya nchi.
Pia Rais ameshamwagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) kuhakikisha anachunguza mapato katika sekta ya madini.
Ndugai katika majibu yake alisema lengo la kamati teule atakayoiunda
ni kupata kufahamu kama taifa linapata nini na wawekezaji wanapata nini
katika biashara hiyo ya mchanga pamoja na biashara yote ya sekta ya
madini nchini.
Jana Kampuni ya Acacia ambayo inachimba madini katika migodi ya
Bulyanhulu na Buzwagi ambayo inasafirishwa kwa wingi makinikia ya shaba,
ilitoa ufafanuzi kuwa makinikia hayo yenye dhahabu, shaba na fedha
yaliyoshikana ndani hayawezi kutenganishwa kwa kutumia sianidi.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa makinikia yanawekwa kwenye makontena ya
tani 20 ambayo kwa satani ya shaba kilo 1,00, kilo 2.5 hadi 3.5 za
dhahabu na kilo 2.5 hadi 3.5 za fedha.
Taarifa ilisema madini hayo yanayosafirishwa yana thamani ya dola za kimarekani 140,000 kwa kontena (sawa na Sh milioni 310).
chanzo:Habarileo.
Comments