Bunge lamwagiza Majaliwa atoe tathmini ya chakula.

BUNGE la Tanzania limemwagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba kutoa tathmini ya hali ya chakula nchini wakati wa majumuisho ya hotuba zao za bajeti.

Agizo hilo lilitolewa bungeni jana na Spika wa Bunge, Job Ndugai wakati akitoa mwongozo wa Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema).

Akiomba mwongozo kwa Spika, Waitara alisema kumeibuka mfumuko mkubwa wa bei ya bidhaa mbalimbali ikiwemo unga wa sembe katika maduka ya miji kadhaa nchini ikiwemo Dar es Salaam, hali inayoleta taswira ya kuwepo kwa njaa nchini.

“Mheshimiwa Spika bei imepanda kwa kiwango kikubwa sana. Kwa mfano, kiroba cha unga ambacho kilikuwa kinauzwa kwa shilingi elfu ishirini sasa kinauzwa kwa kati ya shilingi orobaini na shilingi elfu orobaini na nane.
“Lakini pia debe la mahindi ambalo miaka yote limekuwa linapanda bei kufikia shilingi elfu ishirini, sasa linauzwa kwa zaidi ya shilingi elfu thelathini. Hii ni dalili ya kuwepo kwa njaa, sasa serikali inaonaje kama itaruhusu mahindi yaliyohifadhiwa kwenye maghala sasa yaanze kusambazwa mitaani ili kusaidia kushusha bei hizi za mahindi na unga ili kuwasaidia wananchi masikini? alihoji.
Akijibu, Spika Ndugai alisema: “Mwongozo wangu kwa suala hili ni kwa hotuba ya Waziri Mkuu tunayoianza leo (jana) izingatie suala hili la njaa. Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati unahitimisha hotuba yako tunaomba ulieleze Bunge tathimini ya hali ya chakula nchini.
“Lakini pia hotuba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi izingatie suala hili ili tujue ukweli wa suala hili kwa manufaa ya wananchi,” alisema Ndugai.
chanzo:Habarileo.

Comments