Bajeti wizara ya Katiba na Sheria yapungua.

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi.WIZARA ya Katiba na Sheria imewasilisha taarifa ya Mpango wa Maendeleo na Makadirio ya Bajeti yake ya Mwaka 2017/18 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ikionesha upungufu wa fedha kwa asilimia nne.

Katika mwaka wa fedha 2016/2017, Wizara hiyo iliidhinishiwa na Bunge bajeti ya Sh bilioni 191.45 na sasa wizara inaomba iidhinishiwe Sh bilioni 159.33 ikiwa na upungufu huo.


Wakati bajeti hiyo ikionesha upungufu huo, baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wamehoji kwanini wizara inaomba bajeti pungufu wakati katika baadhi ya ofisi za taasisi zilizo chini yake, ikiwemo ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) visiwani Zanzibar, Pemba, inapelekewa fedha za matumizi mengineyo (OC) ya Sh 100,000 tu kwa mwezi.

Akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya Kamati hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema katika bajeti ya mwaka jana hadi kufikia Desemba 2016, walikuwa wamepokea Sh bilioni 97.2 sawa na asilimia 51 ya bajeti nzima.

Profesa Kabudi alisema mwaka huu wa fedha kumekuwa na upungufu kwa kuwa bado katika fedha zinazotolewa na wahisani na washirika wa maendeleo, hazijajumlishwa katika bajeti kwa kuwa bado mazungumzo yanaendelea.

“Mtakumbuka juzi hapa tulikuwa na ugeni wa Rais wa Benki ya Dunia na Rais wetu, John Magufuli alieleza hilo, sasa haya ni baadhi ya mazungumzo yanayoendelea na matumaini ni makubwa,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema sababu nyingine ya kupungua kwa bajeti hiyo ni ukomo wa bajeti kupungua kwa asilimia 55 lakini ongezeko limekuwepo kwa asilimia 11 katika fedha za mishahara na Fedha za OC kwa asilimia 26 mwaka 2017/2018.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo akiwemo Mbunge wa Malindi, Ali Saleh Ali (CUF) na Mbunge wa Viti Maalum, Riziki Lulida (CUF) walihoji kwa nini ofisi ya THBUB haiboreshewi fedha za OC na kuifanya kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Saleh alisema walipotembelea visiwani Pemba hivi karibuni, walikuta fedha ya OC katika ofisi hiyo kwa mwezi ni Sh 100,000 huku kukiwa na mtumishi mmoja katika ofisi ambaye anafanya kazi zote kazi za Tume, usimamizi na usafi wa ofisi.

“Hatumtendei haki kiongozi wa hii tume, haiwezekani tume inayosimamia masuala ya haki za watu nchini na ndio mwakilishi wetu kimataifa wa haki hizo haboreshewi OC, hii si sawa kabisa,” alisema Lulida.
chanzo:Habarileo.

Comments