Awamu ya 3 mradi kusambaza umeme vijijini yazinduliwa.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani akibonyeza kitufe kuwasha kifaa maalumu cha Umeme Tayari (UMETA) katika kijiji cha Negezi, kata ya Ukenyenge wilayani Kishapu jana, wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusambaza umeme vijijini kwenye mkoa wa Shinyanga. (Na Mpigapicha Wetu).NAIBU Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani amezindua mradi wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu katika Mkoa wa Shinyanga wilayani Kishapu jana wenye thamani ya Sh bilioni 35.5.
Katika uzinduzi huo uliofanyika Kijiji cha Negezi, Kata ya Ukenyenge wilayani Kishapu, ukihusisha vijiji 149, Dk Kalemani aliagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikishwa wanasambaza umeme sehemu zote bila upendeleo.

Aliwahimiza wananchi kutumia fursa ya kuwepo kwa nishati hiyo katika kuboresha maisha yao kwa kutumia miradi ya uzalishaji mali pamoja na huduma mbalimbali za kijamii.
Aliwataka wautumie kwa kujenga viwanda vya kusindika mazao pamoja na huduma za afya, elimu, maji na viwanda vingine kama mashine za kusaga ambazo zitawapatia kipato na kuboresha maisha.
Aidha, Dk Kalemani alizitaka serikali za kata na vijiji kubainisha maenbeo maalumu ya viwanda ambayo katika mradi huo yatafikishiwa miundombinu ya umeme mkubwa.
“Tunataka kuwezesha wajasiriamali vijijini kupatiwa umeme utakaowezseha kuanzishwa kwa viwanda vidogo na vikubwa vijijini kwa gharama nafuu,” alisema Dk Kalemani.
Aliongeza kuwa wananchi watakaounganishiwa umeme wanatakiwa kukamilisha utandazaji wa nyaya katika nyumba zao mapema ili mkandarasi akifika wawe tayari kulipia na kuunganishiwa umeme.
Alisema kwa sehemu ambazo utandazaji utakuwa haujakamilika au nyumba si kubwa wanahimizwa kuomba kufungiwa kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) ambacho hakihitaji kutandaza nyaya.
chanzo:Habarileo.

Comments