Ataja sababu wasichana kuwa watoro shuleni.

MKURUGENZI wa shirika lisilokuwa la serikali la Thubutu Africa Initiative (TAI), Jonathan Kifunda amesema kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wasichana nchini wanaingia kwenye hedhi bila kuwa na elimu ya afya yoyote, hali inayosababisha utoro shuleni.

Hata hivyo alidai wamekuwa wakipoteza muda wa masomo kwa zaidi ya siku 45 kwa mwaka wakiwa katika hali hiyo. 

Mkurugenzi huyo aliyasema hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa mradi mpya ujulikanao kama ‘usichana wangu kwanza’ unaolenga kuwaelimisha wazazi na watoto wa kike pamoja na kutatua matatizo yanayowapata wanafunzi shuleni kwa kipindi cha hedhi.


Kifunda alisema kuwa mradi huo wenye lengo la kutoa elimu kwa wanafunzi wa kike wa shule za msingi na sekondari ambapo wamekuwa wakiingia kwenye kupevuka bila kuwa na elimu ya afya, hali ambayo imekuwa ikiwapa hofu na woga na kuwa watoro shuleni. 

“Kupitia mradi wa usichana wangu tutahakikisha tunatoa elimu ya afya kwa wazazi na wanafunzi na kuzipunguza changamoto ikiwa imebainika zaidi ya asilimia 80 ya wasichana nchini wanaingia kwenye hedhi bila kuwa na elimu ya afya yoyote , matokeo yake wanajawa na hofu kubwa na woga, hali ambayo inasababisha utoro mashuleni,” alisema.

Baadhi ya walimu akiwemo mwalimu kutoka shule ya sekondari Kishapu, Stephen Cleophas alisema kuwa muda mrefu changamoto hiyo imekuwa ikisababisha wanafunzi wa kike kufanya vibaya katika masomo huku wakiiomba serikali kushirikiana na wadau kuielimisha jamii juu ya changamoto hiyo kwani imekuwa ikishusha kiwango cha elimu kwa wanafunzi wa kike.

 Ofisa Elimu Mkoa wa Shinyanga, Mohamed Kahundi alikiri kuwepo kwa utoro mkubwa kwa wanafunzi wa kike shuleni, hali aliyoielezea ni ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi kwa watoto wa hao.

Alisema bado kuna tatizo la upatikanaji wa vitambaa vya kujisitiri wanafunzi wa kike shuleni kwani bajeti inayotolewa na serikali hatoshelezi mahitaji. “Asilimia 10 ya fedha za huduma ya kwanza katika shule, haitoshi kuhudumia wanafunzi wote kwani shule zina wanafunzi wengi ikiwa tunaendelea kuangalia namna ya watoto hawa ili waweze kuhudhuria masomo yao,” alisema.
chanzo:Habarileo.

Comments