MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameishauri serikali itafute vyanzo mbadala vya mapato ya ndani, badala ya kutegemea fedha za wahisani, ambazo baadhi hazitolewi na hivyo kuathiri miradi ya maendeleo.
Pia mdhibiti huyo ameitaka serikali kuendelea kuziba mianya mbalimbali, inayotumika kukwepa kulipa kodi na kuboresha udhibiti wa ndani katika mifumo ya ulipaji kodi ambayo itasaidia wafanyabiashara na kufanya kazi zao kwa uhuru na kulipa kodi kwa hiari.
CAG ametoa ushauri huo baada ya kubaini kuwa fedha za maendeleo zilizoahidiwa na baadhi ya washirika wa maendeleo, hazikutolewa hivyo kuathiri miradi mingi nchini.
“Kuendelea kutegemea washirika wa maendeleo ambao wanatoa fedha kwa masharti na wakati mwingine hawatoi kabisa kunaweza kuchelewesha matokeo tunayotegemea kwa wakati,” inasema ripoti hiyo ya CAG. Alitoa mfano kuwa katika mwaka wa fedha 2015/16, Tanzania ilitegemea kupokea kutoka akaunti ya Changamoto za Milenia Tanzania (MCA (T) kiasi cha Sh bilioni 347.80, lakini hawakutoa fedha yoyote.
Pia nchi ilitegemea kiasi cha Sh bilioni 660.34 kutokana na misaada na mikopo yenye masharti nafuu ya kibajeti ila kilipatikana kiasi cha Sh bilioni 291.38 (sawa na asilimia 44 ya lengo kusudiwa). “Hii ina maana shughuli zote za maendeleo zilizopangwa kutekelezwa kwa kutumia fedha hizo hazikutekelezwa,” ilifafanua ripoti hiyo. Kuhusu kodi, CAG ameishauri serikali, kupitia mamlaka ya nidhamu kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wafanyakazi wasio waadilifu pamoja na kuboresha udhibiti wa ndani katika mifumo ya ulipaji kodi, ambayo itasaidia wafanyabiashara na kufanya kazi zao kwa uhuru na kulipa kodi kwa hiari.
Pia, kuhakikisha matumizi bora ya mifumo wa kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ili kuongeza ufanisi na kupunguza upotevu wa mapato. Udhibiti na uhamasishaji zaidi juu ya matumizi ya vifaa vya kielektroniki katika kukusanya mapato, kwani wengi wamekuwa hawatumii vifaa hivyo kwa madai ya matatizo ya kimtandao. “Makusanyo ya mapato ya ndani yameonesha mwenendo chanya katika kipindi cha miaka minne mfululizo.
Pamoja na makisio ya mapato kuongezeka na ukusanyaji wa mapato kukua, bado kumekuwa na changamoto kama vile bajeti kupunguzwa,” inasema ripoti hiyo. Ripoti imefafanua kuwa fedha nyingi kutolewa mwishoni mwa mwaka wa fedha na kutofikia malengo ya makusanyo kusudiwa. Imesisitizwa kuwa bila ya kuwa na bajeti halisi, malengo ya uendeshaji na ya kimkakati ya taifa yatafikiwa kwa kutumia mikopo.
Kuhusu eneo la usimamizi wa rasilimali watu, CAG ametaja kasoro alizobaini katika eneohilo kuwa ni kuwa kuwepo kwa watumishi wengi kukaimu nafasi zaidi ya muda unaokubalika kisheria, posho ya kukaimu nafasi mbalimbali kutokukatwa kodi, upungufu wa watumishi, baadhi ya taasisi kushindwakufanya tathmini na kupima utendaji wa watumishi.
Dosari nyingine ni katika utunzaji wa kumbukumbu za watumishi, kutokulipa stahili mbalimbali za watumishi na baadhi ya waajiri kushindwa kuijulisha Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kuhusu wanufaikaji na kuanza kuwakata na kuwasilisha makato hayo Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. “Mapungufu katika usimamizi wa rasilimali watu yanaathiri ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya serikali,” inasema ripoti hiyo.
Katika eneo la manunuzi ya umma, CAG ameishauri serikali kuzingatia sheria ya manunuzi ya umma ili kuepuka kujirudia kwa mapungufu yaliyobainika. CAG amependekeza serikali kupitia Wizara ya Fedha itenge fedha za kutosha kuweza kugharamia miradi ambayo haijakamilika kutokana na kukosa fedha za kutosha. Serikali itekeleze miradi mikubwa kwa awamu ili kuepuka gharama za ziada zinatokana na tozo za kuchelewesha malipo kwa makandarasi.
chanzo:Habarileo.
Comments