Afrika Kusini hii leo inatazamiwa kupanda kizimbani katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kutoa sababu za kutomkamata Rais Omar al-Bashir wa Sudan alipoitembelea nchi hiyo miaka miwili iliyopita.
Wahanga kadhaa wa mauaji ya kimbari ya Darfur ambao kwa sasa wanaishi Uholanzi watafuatilia kwa karibu kesi hiyo.
Monica Feltz, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la International Justice Project amesema manusura kadhaa wa mauaji ya kimbari ya Darfur wanafuatilia kuanza kwa vikao hivyo, wakiwa na matumaini ya kupata haki waliyopigania kwa miaka mingi.
Rais wa Sudan anatuhumiwa na ICC kuwa alihusika na jinai na mauaji ya kimbari huko Darfur magharibi mwa nchi hiyo mwaka 2003.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu zaidi ya laki 3 wameuawa hadi kufikia sasa katika jimbo la Darfur, huku wengine milioni 2.5 wakilazimika kuwa wakimbizi.
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC iliyoko mjini The Hague nchini Uholanzi imetoa waranti wa kukamatwa al-Bashir mara mbili, mwaka 2009 na 2010. Hata hivyo nchi nyingi hususan za Afrika zimekataa kumkamata na kumkabidhi kwa ICC rais huyo wa Sudan, alipozitembelea.
chanzo:parstoday.
Comments