
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Balozi wa Tanzania Nchini India Balozi Mohamed Hija wakati akikiongoza Kikao cha matayarisho cha Ujumbe wa Zanzibar
Balozi Mohamed Hija alisema Zanzibar ina fursa pana ambazo
bado haijazitumia katika kujitanua kimawasiliano kwa kushirikiana
na Taasisi mbalimbali Duniani katika harakati zake za
kujikwamua kiuchumi na kuimarisha mipango yake ya Maendeleo hasa kwenye
zile Sekta zilizo nje ya Muungano.
Alisema India imebarikiwa kuwa na Taasisi na Makampuni mengi kwenye Serikali za Majimbo ambazo zinaweza kusaidia nguvu za Kiuchumi Visiwani Zanzibar iwapo mipango ya uhakika itawekwa ukiwemo utaratibu maalum wa kufuatilia makubaliano yanayofikiwa ya pande mbili husika.
Balozi Hija aliueleza Ujumbe huo wa Zanzibar kwamba Ofisi ya Ubalozi Nchini India iko tayari kuratibu masuala yote yatayohusika na mikataba au makubaliano baina na Zanzibar na Taasisi au Serikali ya Jimbo lolote Nchini humokatika uanzishwaji wa ushirikiano wa kisekta.
Alifahamisha kwamba ipo miradi inayofikia hatua ya kutiwa saini katika uanzishwaji wake lakini kinachokosekana kuibuka kwa miradi hiyo na hatimae mengine kufifia ni ukosefu wa ufuatiliaji wa miradi hiyo jambo ambalo huwavunja moyo wale wanao nia thabiti ya kusaidia.
Balozi Hija alielezea faraja yake kutokana na ujio wa Ujumbe huo wa Zanzibar Nchini India na kusema kwamba huo ni mwanzo mzuri wa kufungua njia itakayotoa mwanga kwa Zanzibar kujitanua zaidi kiuchumi Kimataifa.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ziara hiyo ina lengo la kutengeneza Diplomasia juu ya ushirikiano kati ya Zanzibar na India hasa katika sekta za Afya, Kilimo, Biashara na hata Utalii.
Balozi Seif alisema India imekuwa mshirika mkubwa wa Zanzibar katika Sekta ya Afya kiasi kwamba wagonjwa wengi wa Zanzibar wanaosumbuliwa na maradhi tofauti kama Moyo, Figo pamoja na magonjwa mengine hupata
huduma za matibabu katika Hospitali za India.
Othman Khamis Ame.
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
19/3/2017.
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
19/3/2017.
chanzo: zanzibar24.
Comments